HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 22, 2016

Mamlaka ya Bandari yashauriwa kuitupia jicho Bandari ndogo ya Kilwa Masoko Na Adili Mhina, Kilwa

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (mwenye kofia) akiambatana na timu ya ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Tume ya Mipango, watumishi wa Bandari ndogo ya Kilwa pamoja na maofisa kutoka Halmashauri ya Kilwa wakielekea ukaguzi wa maeneo mbalimbali katika  Bandari ya Kilwa Masoko. 
 3. Kivuko kilichopo katika Bandari ya Kilwa Masoko ambacho hakitumiki mara kwa mara ambapo wanachi hutumia boti zinazotoza nauli ya shilingi 1,000.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri akiulizia juu ya utendaji kazi wa kivuko (hakipo pichani) wakati wa ziara ya Tume ya Mipango katika Bandari ndogo ya ya Kilwa masoko.


Mamlaka ya Bandari imeshauriwa kuiangalia bandari ndogo ya Kilwa Masoko katika kuboresha miundombinu na vitendea kazi ili kuongeza ufanisi wa shughuli bandari hapo ikiwa ni njia mojawapo ya kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara nchini. 

Ushauri huo umetolewa hivi karibuni na Kaimu Katibu Mtendaji kutoka Tume ya Mipango Bibi Florence Mwanri alipoiongoza timu ya wataalamu wa ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Tume ya Mipango kukagua shughuli za maendeleo katika bandari hiyo.

Katika ziara hiyo, Mwanri alionesha kutoridhishwa na utendaji kazi wa bandari hiyo baada ya kubaini kuwa hakuna tishari wala  vifaa vinavyoweza kutumika katika kupakia na kupakua mizigo huku akielezwa kuwa mfanyabiashara anapoleta meli banadarini hapo analazimika kutafuta vifaa vya kupakulia mizigo yake mwenyewe. 

“Bandari hii ni fursa kubwa kiuchumi haipaswi kuwa katika hii wakati Serikali ya sasa inajitahidi kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara. Hivyo, ni muhimu kwa Mamlaka ya Bandari kupitia bajeti yao kuangalia  uwezekano wa kupata vifaa hivyo ili kuondoa usumbufu na gharama kwa wafanyabiashara wanaotumia bandari hii,” alisema.

Alieleza kuwa kwa sasa bandari hiyo inaweza kufanya vizuri na kuwa na uwezo wa kujiendesha yenyewe kama mazingira yake yataboreshwa kwa kuwa shughuli za usafirishaji zinaweza kuchangamka baada ya kiwanda cha saruji kujengwa eneo hilo huku kiwanda cha mbolea na kiwanda cha kuchakata  mihogo vikitarajiwa kujengwa Kilwa. 

Alieleza kuwa uwekezaji katika eneo hilo ni muhimu kwani bandari hiyo pia inatumika kusafirisha watalii kutoka ndani na nje ya nchi  kutokana na kuwepo vivutio mbalimbali vya utalii katika Wilaya ya Kilwa.

Hata hivyo, Mwanri alisisitiza kuwa kabla ya kufanya uwekezaji mkubwa bandarini hapo ni lazima ufanyike upembuzi yakinifu ili kuwa na taarifa za kisayansi juu ya aina ya uwekezaji unaohitajika. Utafiti wa soko pia unahitajika kuweza kubaini fursa za kibiashara zinazoweza kupatikana ikiwa uwekezaji mkubwa utafanyika. 

Bandari ya Kilwa Masoko inaelezwa kuwa ipo katika mazingira mazuri kijiografia kwa kuwa eneo hilo la bahari halina upepo mkali unaoweza kuleta usumbufu wakati meli zinapotia nanga. Vile vile bandari hiyo ipo karibu na Dar es Salaam hivyo inaweza kutumika kusapunguza mlundikano wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam.

Tofauti na bandari zingine, Bandari ya Kilwa Masoko inaelezwa kuwa na kina kirefu zaidi ambapo katika lango la lake kuna kina cha takribani mita 60 hivyo meli kubwa zinaweza kufika bandarini hapo bila  kuingia gharama za uchibaji kwa ajili ya kuongeza kina. 

No comments:

Post a Comment

Pages