HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 11, 2016

Msama atoa ya moyoni

NA MWANDISHI WETU

MENEJA wa zamani wa malkia wa nyimbo wa injili nchini, Rose Muhando, Alex Msama amesema hana chuki wala kinyongo na mwimbaji huyo licha ya kufanyiwa visa na vituko ikiwemo madai kwamba amemtumia kuvuna fedha na utajiri huku yeye akibaki masikini.

Akizunguza jijini Dar es Salaam, Msama aliyechangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa muziki wa injili nchini kupitia matamasha ya muziki huo tanngu mwaka 2000 hasa Pasaka, alisema ameshangazwa na madai ya Rose aliyotoa hivi karibuni kupitia chombo kimoja cha habari.

Msama alisema katika mazingira ya kawaida, ni vigumu kusema amemtumia Rose kupata utajiri kwani wakati anaanza kuandaa tamasha la Pasaka la kwanza mwaka 2000, tayari alikuwa na uwezo kifedha wa kufanya jambo hilo wakati huo mwimbaji huyo hajulikani.

Alisema kwa kadiri tamasha hilo lilivyozidi kupata umaarufu ndani na nje ya Tanzania kupitia kuwatumiwa waimbaji wa hapa nchini na kutoka nje, ndivyo umaarufu wa waimbaji mbalimbali waliokuwa wakishirikishwa akiwemo Rose, ukazidi kupanda.

“Katika mazingira ya kawaida, mwimbaji aliyekuwa akipewa nafasi ya kuimba katika tamasha la Pasaka na kulipwa fedha kwa mujibu wa makubaliano, iweje leo hii aseme alitumika bure wakati kila Tamasha alilipwa fedha?,” alihoji Msama.
Msama amekwenda mbali na kumsihi Rose kuangalia alipojikwaa kwa kujirekebisha mwenendo na staili ya maisha yake kwa sababu sio kwamba hapati fedha, bali ni aina ya matumizi na staili ya maisha anayoishi yanayomlazimu atumie fedha nyingi kwa siku.

Alisema kama Rose ataweza hilo, anaamini bado lipo ndani ya uwezo wake, maisha yake yatabadilika kwani bado ni mwimbaji aliyepo katika kiwango bora akiwa na kipawa cha aina yake katika huduma ya uimbaji.

Msama alisema ni vigumu leo hii mwimbaji aliyeshiriki matamasha yaliyowahi kuandaliwa na kampuni yake ya Msama Promotions akasema alitumika kumtajirisha kwa sababu; alifanya hivyo kwa makubalino maalumu ya malipo na kupewa ujira wake, hivyo kama ni faida ilikuwa kwa pande zote mbili.

Alipoulizwa kwanini alijivua nafasi ya kuwa Meneja wa mwimbaji huyo, Msama alisema sababu kubwa ni baada ya mwimbaji huyo maarufu kuanza kuandamwa na kashfa ya kupokea fedha za watu kwa ajili ya kwenda kuhudumu na kutofanya hivyo.

Alisema ingawa hata yeye ameshawahi kumlipa Rose kila kitu na kukacha, kilichomuuma zaidi ni kwamba malalamiko yalikuwa yakija kwake na kutatua ikiwemo kurejesha fedha za watu ambazo walizitoa bila mwimbaji huyo kwenda kuhudumu.

Msama alisema pamoja na udhaifu huo wa Rose ambao anaamini bado anayo nafasi ya kurejea kwenye mstari kama akiamua huku akimtanguliza Mungu na kuongeza ingawa kwa sasa si Meneja wake, amekuwa akiuza kazi zake nyingi na kusema hana kinyongo wala chuki naye.

No comments:

Post a Comment

Pages