Wanachama wa Simba wakiomba dua kabla ya kuanza kwa mkutano. (Picha na Francis Dande).
Rais wa klabu ya Simba, Evans Aveva, akizungumza na wanachama katika Mkutano Mkuu wa dharura wa mabadiliko katika Katiba ya Simba Ibara ya 49 uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Wachama wakipitia taarifa.
Mzee Hassan akitoa ya moyoni wakati wa mkutano huo.
Wanachama wa Simba wakipiga kura kupitisha mabadiliko ya kifungu cha Katiba.
Kura zikipigwa.
Wanachama wakiunga mkono mabadiliko.
Simba Oyeee, Rais wa Simba Evans Aveva.
Na Mwandishi Wetu
Wanachama wa klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam,
hatimaye wamebariki mabadiliko ya kimfumo kutoka uendeshaji wa kawaida
hadi kuwa wa muundo wa hisa, baada ya kupitisha kipengele kinachoruhusu kuanza
kazi kwa mfumo huo mpya.
Mabadiliko hayo, ambayo awali yalipitia mapingamizi
kadhaa ya Serikali, Shirikisho la Soka na baadhi ya wanachama wa Simba, umefanyika katika Mkutano Mkuu wa Dharura wa wanachama uliokuwa na agenda ya
mabadiliko ya katiba.
Simba imelazimika kuitisha Mkutano Mkuu wa Wanachama
kubadili mfumo huo, ili kutii agizo la Serikali kuitaka iratibu mchakato sahihi,
ili kuipa fursa ya kuuza kwa Sh. Bil. 20 asilimia 51 ya hisa zake kwa Mohammed
Dewji ‘Mo’, ambaye ameshaanza uwekezaji ndani ya klabu hiyo.
Jumla ya wanachama 642 walishiriki katika mkutano
huo uliofanyika katika Bwalo la Maofisa wa Polisi, Osterbay, Dar es Salaam,
ambako mabadiliko yalipitishwa kwa asilimia 98 ya wanachama hao, huku wachache
wakiyapinga.
Mkutano huo ulioendeshwa na Rais wa Simba, Evance
Aveva, ambako wanachama walikuwa watulivu kwa kufuata kipengele kwa kipengele,
hasa cha kuwepo kwa muundo huo, ambako wameongeza kipengele ndani ya katiba ya
Simba ibara ya 49.
Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, Ibara hiyo ya 49,
inazungumzia: kubadilisha mfumo, kuvunja au kufutwa kwa Simba Sports Club,
ambako wanachama walipitisha kipengele
hicho kwa pamoja na vipengele vingine vyote vidogo vilivyomo ndani ya Ibara
hiyo.
Kipengele kidogo cha 49(i), kinasomeka kuwa: Uamuzi
wowote wa kubadilisha mfumo, kuvunja au kufutwa kwa Simba SC, unahitaji
theluthi mbili (2/3) ya wanachama wote wa Simba waliopatikana katika Mkutano
Mkuu uliopitishwa maalum kwa madhumuni hayo.
Kipengele cha 49(ii), kinasomeka kuwa hakutakuwa na
mabadiliko na kipengele cha 49(iii) kinasomeka kuwepo na sababu za kubadilisha
mfumo, kuvunja au kufutwa kwa Simba kama vile kuwa na madeni makubwa yasiyolipika,
kupoteza hadhi ya kutoaminika na kukopesheka au kuendana na matakwa ya mfumo wa
nyakati za biashara.
Katika ibara 49(a), kipengele kilichopitishwa
kinasema: Mkutano wa Wanachama unaweza kuitishwa kwa mujibu wa Ibara ya 22 na
kufanya mabadiliko ya mfumo wa umiliki au uendeshwaji wa Simba, wakati
kipengele (b) kinasema:
Mabadiliko ya mfumo wa uendeshwaji au umiliki wa Simba hayataathiri hadhi ya wanachama wote halali wa Simba.
Mabadiliko ya mfumo wa uendeshwaji au umiliki wa Simba hayataathiri hadhi ya wanachama wote halali wa Simba.
Pia uwiano wa thamani ya umiliki wa kila mwanachama
katika mfumo mpya utajadiliwa na Kamati ya Utendaji kutokana na thamani ya
klabu na uwekezaji.
Kipengele (c) cha ibara hiyo kinaeleza kuwa; Mfumo
mpya wa mabadiliko ya uendeshaji au umiliki wa Simba utarithi haki na mali zote
pamoja na madeni na wajibu wowote uliokuwa chini ya Simba kabla ya mabadiliko
hayo.
Katika kipengele (d) na cha mwisho cha Ibara hiyo, kinasema:
Mabadiliko ya mfumo wa umiliki au uendeshaji wa Simba yatabainisha kuacha
kutumika kwa katiba hii na mkutano mkuu chini ya mfumo mpya utapitisha katiba
mpya chini ya utaratibu wa haki na kura za mfumo huo mpya.
Wanachama hao kwa pamoja waliamua kupitisha
kipengele hicho ambapo Rais Aveva amewataka kuwa watulivu kwa kuwa mabadiliko
hayo sasa yatawasilishwa kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wizara ya
Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo na mwisho kwa Msajili wa Vyama na Klabu za
Michezo, kabla ya kuwa katiba kamili.
No comments:
Post a Comment