Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme - TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu akizungumza na watumishi wa karakana za TEMESA wakati akifungua mafunzo kwa watumishi hao Jijini Dar es Salaam. |
Na Theresia Mwami TEMESA
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme - TEMESA Dkt. Mussa
Mgwatu leo amefungua mafunzo elekezi kwa watumishi wa karakana juu ya mfumo wa
utozaji gharama za matengenezo ya magari katika karakana za TEMESA pamoja na
mfumo wa utoaji taarifa za uzalishaji na matengenezo za kila mwezi.
Dkt. Mgwatu amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuleta uwiano sawa
katika gharama za matengenezo ya magari kwa karakana zote za TEMESA bila kujali
mikoa zilipo karakana hizo.
Aliongeza kuwa utaratibu utakaoelekezwa katika mafunzo hayo utasaidia
kupunguza gharama za matengenezo ya magari ya serikali, suala linalolalamikiwa
na wateja wa TEMESA kwa muda mrefu sasa.
“Nataka sasa tuanze kutoza gharama za matengenezo ya magari
kulingana na muda unaotumika kutengeneza gari husika (man hour), badala ya
kutumia kigezo cha asilimia ya fedha iliyotumika kununulia vipuri kwa ajili ya
matengenezo ya magari, kwani baadhi ya vipuri ni ghali sana lakini hutumia muda
mchache sana kuvifunga,” alisema Dkt. Mgwatu.
Dkt. Mgwatu alisema kuwa, kumekuwa na changamoto ya uwasilishaji
wa taarifa za utendaji kutoka katika
mikoa/vituo vya TEMESA, mara nyingi taarifa hizi hazifiki kwa wakati. Huku
akisisitiza kuwa ni matumaini yake baada ya mafunzo hayo taarifa hizo zitakuwa
zikifika kwa wakati tena zikiwa sahihi.
Aidha Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Matengenezo,
Mhandisi Sylivester Simfukwe alisema idara yake imejipanga kutoa huduma bora zinazokidhi
viwango hasa katika matengenezo ya magari ya serikali, ili kuhakikisha kuwa
uzalishaji unaongezeka na kero za wateja zinakwisha.
Aliongeza kuwa mafunzo
kama hayo yatatolewa kwa wawakilishi wa karakana zote za TEMESA nchi nzima.
Mafunzo hayo elekezi juu ya Mfumo wa utozaji gharama katika
karakana za TEMESA pamoja na mfumo wa utoaji taarifa za kila mwezi, yanafanyika
kwa siku 5 katika ukumbi wa MT. Depot, Dar es salaam na yamehusisha watendaji
wa TEMESA kutoka mikoa ya Tanga, Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Lindi na
Mtwara, pamoja na vituo vya MT. Depot na Kikosi cha Umeme.
No comments:
Post a Comment