Na Luteni Selemani Semunyu JWTZ
Klabu ya Golf ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ya Lugalo iko katika maandalizi ya viwanja kwa ajili ya mashindano ya kuadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo mwaka 2006.
Akizungumza na waandishi wa Habari msimamizi wa viwanja ambaye pia ni mchezaji wa kulipwa wa klabu ya Lugalo David Helela alisema kila kitu kinaenda sawa na wanaangalia sehemu ngumu kuchezeka kuondoa vikwazo visivyo na sababu.
“kuna vikwazo vinavyopaswa kuwepo katika Uwanja wa golf lakini kuna vikwazo vingine vinakuwepo lakini havina sababu wala havina mchango katika kuonyesha umahiri wa mchezaji hivyo tunaviondoa”, Alisema Helela.
Aliongeza kuwa mbali na kuviondoa bado viwanja kama namba 12 vitaendel;ea kuwa moja ya kiwanja kigumu kwa mchezaji atakayecheza katika uwanja huo kutoka na jinsi ulivyowekwa kwa lengo tu la kukamilisha sifa za uwanja wa Golf.
Helela Alisema katika kuelekea kuadhimiasha Miaka 10 klabu ya lugalo itabaki kuwa ndio klabu pekee inayothamini kwa kiwango kikubwa mchango wa wachezaji wa kulipwa ambao mbali na kuwatumia katika kufundisha vijana na kusimamia sheria za mchezo lakini wamekuwa wakishirikishwa katika mashindano ya wachezaji wa kulipwa .
Kwa Upande wake Afisa Tawala wa Klabu hiyo Kapteni Amanzi Mandengule alisema amefanya ukaguzi wa Awali kazi zinaenda vizuri na kutoa wito kwa wadhamini kuongeza nguvu ili kuwa na mashindano Bora.
“ Kuna wadhamini tuliofanikia na wako tayari na wameanza maandalizi lakini Milango iko wazi kwa wadhamini wengine kujitokeza kwani Mashindano ya Miaka 10 ya Klabu yanatarajiwa kuwa ya Aina yake ukilinganisha na mashindano yaliyowahi kuandaliwa”Alisema kapteni Mandengule.
Aliongeza kuwa taarifa rasmi ya mashindano na Mgeni rasmi inatarajiwa kutolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Klabu Brigedia Jenerali Michael Luwongo ili kuelezea kwa kina mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika katikati ya Mwezi wa Pili.
Katika mashindano hayo yanayotarajiwa kuwa ya siku tatu Vilabu vyote vimealikwa na makundi yote ya mashindano yatashirikishwa katika mashindano hayo ambayo yatakuwa ni mashindano ya Kwanza makubwa nchini kwa mwaka 2017 .
No comments:
Post a Comment