WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha inawasaka watu wote waliohusika na upotevu wa mali za kiwanda cha chai cha Lupembe na kuwachukulia hatua.
Hata hivyo amesema Serikali haitoipa nafasi migogoro yote ya uwekezaji inayopelekea wananchi kutopata ajira bali itatatuliwa bila ya kusimamisha uzalishali.
Pia amewataka wawekezaji mbalimbali waliomilikishwa viwanda wahakikishe wanafuata kanuni na sheria ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na wananchi waweze kupata tija.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Januari 25, 2017) wakati alipotembelea kiwanda cha chai cha Lupembe akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Njombe.
Mali za kiwanda hicho vikiwemo vipuli na vyombo vya usafiri yakiwemo maroli na magari madogo 17 vilipotea baada ya Ushirika wa wakulima wa chai Muvyulu kuvamia kiwanda.
Kiwanda hicho kinakabiliwa na mgogoro kati ya muwekezaji wa kiwanda hicho Lupembe Tea Estate na Ushirika wa wakulima wa chai Muvyulu ambao ameahidi kuitafutia ufumbuzi.
“Migogoro yote inayopelekea watu kutopata ajira haitapewa nafasi. Tutaisikiliza na kuipatia ufumbuzi bila ya kusimamisha uzalishaji,”.
“Ushirika nchini uliyumba na umekuwa ukiharibiwa na waliopewa dhamana na ndiyo sababu tuliamua kuufumua uongozi kuanzia juu na tutashuka hadi chini,” amesema.
Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kufuatilia viongozi wa vyama vya ushirika na wenye uwezo wa kuviendesha wataendelea na wasioweza wataondolewa.
Amesema Serikali itayafanyia kazi maelezo yote yaliyotolewa na uongozi wa kiwanda hicho pamoja na ya wanaushirika na kisha itayatolea ufafanuzi wakati kiwanda kikiendelea na kazi.
Waziri Mkuu amesema Serikali itahakikisha mwenye haki anapata haki yake na haitakubali kuona kiwanda hicho kikisimamisha uzalishaji. Pia inafuatilia muwekezaji huyo alipataje kiwanda.
“Lupembe ni miongoni mwa viwanda ambavyo vilikufa na sasa kimeanza uzalishaji hatutakubali kife kutokana na migogoro ya wanaushirika na muwekezaji. Kiwanda hakitasimama ng’o,”.
“Hatuwezi kukubali migogoro iendelee kwani haina tija inaumiza wananchi. Najua ushirika ni wa wakulima tunataka uwe imara hatutaki ushirika wenye mizengwe mizengwe,” amesema.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuja na kufanya uchunguzi wa kiwanda hicho.
Amesema Serikali imedhamiria kuwaletea wananchi maendeleo na haitamvumilia mtu atakayevuruga uendeshaji wa viwanda. “ Tunataka viwanda vifanye kazi”
Waziri Mkuu amesema Serikali imedhamiria kupiga hatua kiuchumi kutoka katika uchumi wa chini hadi wa kati kwa kupitia sekta ya viwanda.
Awali Waziri Mkuu alipokea taarifa ya kiwanda hicho kutoka kwa muwekezaji pamoja na taarifa ya uongozi wa Ushirika wa wakulima wa chai Muvyulu ambao ameahidi kuitafutia ufumbuzi.
Waziri Mkuu leo ameendelea na ziara yake mkoani Njombe baada ya kuikatiza Januari 22 mwaka huu na kwenda mkoani Dar Es Salaam kwa shughuli za kikazi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, JANUARI 25, 2017.
No comments:
Post a Comment