Na Lilian Lundo, MAELEZO-Dodoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema kwamba Tanzania haitapata upungufu wa sukari kutokana na kuanza kwa uzalishaji wa sukari kwa viwanda vya ndani.
Waziri Mkuu ameyasema hayo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge Suleiman Ahmed Sadick alipotaka ufafanunuzi namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga ikiwa tatizo la upungufu wa sukari litajirudia tena.
“Tayari Viwanda vya ndani vimeanza uzalishaji wa sukari ambapo kufikia mwisho wa mwezi Machi mwaka huu ambao ndio mwisho wa msimu tutakuwa tumefikia lengo la uzalishaji wa sukari kwa nchi nzima,” alifafanua Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka wafanyabiashara kutoweka vyakula ndani ili kuviuza kwa bei ya juu baadae, badala yake amewataka kuuza vyakula hivyo ili kuongeza upatikanaji wa chakula nchini, kwani uongezaji wa bei wa vyakula unaumiza wananchi wa kipato cha chini na kati.
Katika kukabiliana na tatizo la ukame kwa baadhi ya maeneo hapa nchini, Waziri Mkuu amewataka wakulima kutumia kipindi hiki ambacho baadhi ya maeneo yanapata mvua kwa kupanda mazao ya muda mfupi ambayo pia mazao hayo yataweza kutumika kwa msimu ujayo.
No comments:
Post a Comment