HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 01, 2017

MAELFU WAMZIKA DAVID BURHAN

Jeneza lililokuwa na mwili wa marehemu David Burhan ambaye alikuwa mchezaji wa zamani wa Mbeya City, Lipuli na Kagera Sugar  likiwa katika uwanja wa Samora tayari kwa ajili ya kuagwa na kuelekea mazishini katika makaburi ya Makanyagio.
Mmoja wa waombelezaji waliojitokeza kuaga mwili wa marehemu David Burhan mchezaji wa Kagera Sugar akilia kwa uchungu baada ya kuaga mwili huo katika tukio lilofanyika uwanja wa Samora na kuhudhuliwa na maelfu ya wakazi wa mkoa wa Iringa na Mbeya.
Baadhi ya mashabiki wa timu ya soka ya Mbeya City waliohudhuria mazishi ya mchezaji wa zamani wa timu hiyo wakiwa makaburini wakati wa mazishi ya mchezaji David Burhan.


NA DENIS MLOWE, IRINGA

MAELFU ya wakazi wa mkoa wa Iringa na vitongoji vyake na mikoa ya jirani wamejitokeza kumzika aliyekuwa mchezaji timu ya soka ya Kagera David Burhan aliyefariki dunia juzi katika hospitali ya Bugando baada ya kuugua ghafla.
 
Wakiongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Sheria na Uanachama wa Shirikisho la Kandanda nchini (TFF), Eliud Peter Mvela ‘Wamahanji’ maelfu wa mashabiki waliojitokeza katika uwanja wa Samora kuaga mwili wa marehemu uliofika majira ya saa nane mchana na kisha katika mazishi yaliyofanyika katika makaburi ya Makanyagio.
 
Wakitoa salamu mbalimbali na ubani baadhi ya viongozi wa soka na vyama mbalimbali walisema kuwa marehemu ameacha pengo ambalo limejidhihirisha kwa umati wa watu waliojitokeza katika kuaga hatimaye mazishi yake wakiwemo mashabiki na viongozi wa timu mbalimbali alizopitia.
 
Akizungumza kwa niaba ya Rais wa TFF, Eliud Mvella alisema kuwa marehemu ameacha pengo katika tasnia ya soka kwa kuwa walitegemea siku moja aje kuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Tanzania kutokana na kiwango chake.
 
Mvella alisema kuwa Burhan alikuwa kipa bora katika msimu wa mwaka 2015/2016 wakati akichezea timu ya Mbeya City ambayo ilikuwa tishio kwa timu zote za ligi kuu alitegemewa sana wa wachezaji vijana waliokuwa wakichipukia hivyo pengo lake ni kubwa na kutoa pole kwa familia.
 
 
 
Mvella ambae  alimwakilisha  Rais  wa TFF , Jamal Malinzi alisema  kuwa TFF  amepokea kwa masikitiko makubwa  kifo cha  mlinda mlango   huyo wa Kagera  Sugar  hasa ukizingatia  kwa msimu  uliopita ndie  alikuwa mlinda mlango bora  akitokea timu ya Mbeya  City .
 
“Tff imesikitika sana kwa kuwa ilikuwa na mipango na David siku baadaye kutokana kuwa na kiwango bora kabisa katika makipa nchi kwa ajili ya timu yaTaifa kwani alikuwa tegemeo sana lakini kazi ya mora haina makosa vizuri ni kuiga yale mazuri aliyokuwa akiyafanya kipindi akiwa hai. “ alisema
 
Kwa upande wake kiongozi wa Msafara kutoka Kagera Sugar, Mohamed Hussein akizungumza kwa niaba ya uongozi wa timu hiyo,alisema kuwa katika watu walioumia kutokana na kifo cha David Burhan basi timu ya soka ya Kagera wameumia kwa kiasi kikubwa kwani hadi mwisho walikuwa nae hadi anaanza kujisikia vibaya.
 
Alisema kuwa mchezaji huyo ameacha pengo kubwa sana kwani kutokana na kiwango chake kwa sasa wamebaki na makipa wawili hali ambayo imeacha pengo kubwa sana kwa timu hiyo na familia kwa ujumla.
 
Aliwapa pole familia ya soka mkoani hapa na familia ya David kwa kumpoteza kijana wao ambaye imeisadia kwa kiasi kikubwa mafanikio timu ya Kagera hadi kufikia kuwa nafasi ya tatu katika ligi kuu ya soka Tanzania Bara.
 
Alisema wakazi wote wa Kagera wamehuzinishwa na msiba huo na wametoa ubani wa shilingi milioni 1 kwa familia ya marehemu na Februari 11 watacheza mechi ya hisani na timu ya Lipuli na mapato yote yataenda katika familia ya David.
 
KUUGUA KWAKE
Taarifa za awali, zinasema kwamba kabla ya umauti, Burhan aliugua ghafla wiki iliyopita akiwa safarini kutoka Singida na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo usiku wa Alhamis.
 
Siku ya Ijumaa alihamishiwa Hospitali ya Kagera Sugar, na kisha kusafirishwa hadi Bugando siku ya Jumapili kwa uchunguzi zaidi. Usiku wa Jumapili, alifanyiwa vipimo na kuonekana kwamba mapafu yamejaa maji. Katika jitihada za kupatiwa matibabu alifariki saa nane za usiku wa Jumapili.
 
Marehemu Burhan ni Mtoto wa mchezaji wa zamani wa Pan Africa, Abdallah Burhan. Alianzia timu ya vijana wa chini ya miaka 20 ya Kagera Sugar, kabla ya kujiunga na Lipuli ya Iringa, Tanzania Prisons na Mbeya City za Mbeya, Maji Maji ya Songea na baadaye kurudi Kagera Sugar hadi mauti yalipomkuta.
 
Marehamu ameacha mke mmoja na watoto watatu ambao walikuwepo katika mazishi katika makaburi ya Makanyagio Mungu amlaze mahala pema.

No comments:

Post a Comment

Pages