HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 01, 2017

MGODI WA BUZWAGI WALIPA KODI ZAIDI YA MIL 700 KWA HALMASHAURI YA MJI WA KAHAMA

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi Asa Mwaipopo(wa pili kutoka kulia) na Meneja Uendelevu wa Mgodi wa Buzwagi ,George Mkanza wakikabidhi hundi ya kodi ya huduma ya zaidi ya Sh Mil 740 kwa Mkuu wa wilaya ya Kahama ,Fadhili Nkurlu(wa pili toka kushoto) tukio lililofanyika juzi mjini Kahama ,Wa kwanza kushoto ni makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Mji wa Kahama Bi Marry Manyambo.
Mkuu wa Wilaya Kahama,Fadhili Nkurlu na akimkabidhi hundi iliyotolewa na Mgodi wa Buzwagi kama Kodi ya Huduma yenye thamani ya zaidi ya Sh Mil 740 , Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama Anderson Msumba kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa hospitali kubwa ya wilaya ya Kahama, mradi ambao ujenzi wake utategemea fedha zinazotokana na kodi za ushuru wa huduma unaolipwa na Mgodi huo.
 Baadhi ya waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kahama wakifuatilia hafla ya kukabidhi hundi kwa halmashauri ya mji wa Kahama.
 Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi Asa Mwaipopo akiwahutubia waheshimiwa madiwani wa halmashauri ya Kahama pamoja na wadau mbalimbali waliohudhuria hafla ya kukabidhi hundi kwa halmashauri ya Mji wa Kahama
 Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu (aliyesimama) akihutubia wageni waalikwa wakati wa hafla ya kupokea hundi ya ushuru wa huduma kutoka Mgodi wa dhahabu wa Buzwagi. Kutokea kushoto waliokaa ni Katibu tawala wa wilaya Kahama Timothy Ndanya na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi Asa Mwaipopo.
 Mkuu wa wilaya Kahama na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi wakiteta jambo.

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii ,Kanda ya Kaskazini.


HALMASHAURI ya mji wa Kahama mkoani Shinyanga imepokea kiasi cha Sh Mil 700,040,000  kutoka kwa kampuni ya Acacia inayomiliki mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi ikiwa ni sehemu ya kodi ya huduma (service levy) ya kipindi cha mwezi Julai na Desemba 2016.

Kiasi hiki ni zaidi ya kilichotolewa kipindi cha Julai na Desemba mwaka 2015 ambapo mgodi huo uliikabidhi halmashauri ya mji wa Kahama hundi yenye thamani ya kiasi cha sh Mil 500,088,000 kama kodi ya huduma ikiwa ni utekelezaji wa sheria kwa kulipa kodi zilizopo kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya Hundi ,Meneja mkuu wa Mgodi wa Buzwagi Mhandisi Asa Mwaipopo alisema Buzwagi inamatumaini makubwa kuwa katika siku za karibuni halmashauri itaanza kutekeleza mradi huo na hivyo kutoa matumaini kwa wananchi wa Kahama kupata huduma nzuri za afya ndani ya wilaya.

“Mpaka sasa kama Kampuni tumekwisha kabidhi kwenu takribani kiasi cha bilioni 1.4 hii ikiwa na maana ya kodi yote ya ushuru wa huduma katika kipindi cha mwaka 2016, wananchi wangetamani kuona mradi huu unaanza maana kiasi hicho kilichopo kama kitatumika kinaweza kutekeleza sehemu kubwa ya mradi huu kwa kuanzia wakati tukisubiri awamu zingine” alisema Mwaipopo.

Katika hafla hiyo ya makabidhiano iliyofanyika katika viwanja vya makazi ya viongozi katika wilaya hiyo,Mwaipopo alisema licha ya Kampuni yake kulipa kodi mbalimbali bado imekuwa ikijishughulisha katika kuhakikisha inakuwa mdau muhimu wa maendeleo kwa kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yanayozunguka Mgodi.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kahama ,Fadhili Nkurlu aliyepokea hundi hiyo kutoka kwa uongozi wa Buzwagi na baadae kuikabidhi kwa mwenyekiti wa halmashauri ya Kahama ameupongeza uongozi wa Mgodi wa Buzwagi kwa jitihada ambazo wamekuwa wakizifanya katika kuhakikisha wanalipa kodi mbalimbali pamoja na jushirikiana na Jamii katika kutekeleza miradi mbalimbali.

Alisema Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi umeekua mstari wa mbele katika kulipa kodi mbalimbali ambako mpaka kufikia sasa zimefikia zaidi ya shilingi bilioni 197 ambazo zimetolewa katika vipindi tofauti.

Akizungumzia matumizi ya pesa hizo katika kutekeleza mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Kahama Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kahama Anderson Msumba alisema halmashauri iko katika hatua za mwisho za utekelezwaji wa ujenzi huo.

Miloni 700,040,000  zilizotolewa zinafanya juma ya pesa zote zilizotolewa katika vipindi vya miaka miwili kufikia Bil 1.2 fedha ambazo zitasaidia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo wa Afya.

No comments:

Post a Comment

Pages