Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma jana. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Dodoma, Jumatano, 1 Februari, 2017:
Serikali imetoa ufafanzi kuhusu
masuala mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa mikopo kwa vijana na malipo ya ada
kwa fedha za kigeni. Ufafanuzi huo umetolewa mjini hapa leo wakati wa kikao cha
pili katika Mkutano wa Sita wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kuwainua Vijana Kiuchumi
Akijibu hoja kuhusu namna
vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini wanavyoweza kufaidika kiuchumi, Naibu
Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Anthony Mavunde, amesema
Serikali imetenga fedha za kutosha kupitia mifuko mbalimbali kuwawezesha vijana
kwa mitaji na mafunzo ya ujasiriamali ili kuwainua kiuchumi.
Ameongeza kuwa vijana
wenyewe ndio wanaopaswa kuchangamkia fursa hizo na pale wanapojiunga katika
vikundi mbalimbali wamekuwa wakipewa mikopo kwa ajili ya mitaji. Alitoa mfano
wa jinsi Serikali ilivyowawezesha vijana waliojiunga na kuwekeza katika viwanda
vidogo vya maziwa na chaki mkoani Simiyu.
Amewataka pia Wabunge na
Halmashauri zote nchini kuendelea kupigania kutengwa maeneo maalum katika sekta
mbalimbali kwa ajili ya kuwapatia vijana na kutengwa kwa asilimia 5 ya mapato
ya Halmashauri kwa maendeleo ya vijana
Ada
kwa Fedha za Kigeni
Serikali imesema, ingawa
haijapokea malalamiko yoyote kuhusu wananchi wasioridhihwa na mtindo wa kutakiwa
kulipa malipo ya ada kwa fedha za kigeni katika baadhi ya shule na vyuo, lakini
imesisitiza kuwa wale wanaotoza ada kwa fedha za kigeni wanakiuka Sheria.
Akitoa ufafanuzi huo, Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhandisi Stella Manyanya amesema kwa mujibu
wa kifungu cha 28 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT), 2006, fedha
inayopaswa kutumika kwa malipo ya huduma nchini ni Shilingi ya Tanzania. Ameviagiza
vyuo na shule nchini kuacha kutoza ada kwa fedha za kigeni na kuhimiza wananchi
watakaobainika kufanya hivyo kutoa taarifa Serikalini.
Si Tatizo Kutumia Majengo UDOM
Serikali imesisitiza kuwa
baadhi ya Wizara zilizoanza kutekeleza agizo la kuhamia Dodoma kutumia baadhi
ya majengo kwa muda kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) hakutaathiri shughuli
za chuo.
Hayo yameelezwa na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama. Waziri Jenista amesisitiza kuwa baadhi ya
Wizara zitatumia majengo ya UDOM kwa sababu mengi ya majengo hayo yalikuwa
hayatumiki kwa sasa kwa shughuli za chuo hicho na hakutakuwa na muingiliano na
shughuli za chuo.
Mradi wa Mabilioni Maji Dar
Serikali kwa kushirikiana
na Mamlaka ya Maji Dar es Salaam imeanza kutekeleza mradi wa usambazaji wa maji
utakaogharimu Dola za Marekani milioni 32.772 ambazo ni mkopo kutoka Benki ya
Exim ya China. Mradi huo utahusisha sehemu yote ya jimbo la Kawe, Dar es
Salaam. Mradi huo utachukua miezi 15.
Imetolewa na: na Idara ya Habari-MAELEZO.
No comments:
Post a Comment