HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 15, 2017

BENKI YA CRDB YATOA TAARIFA YA MWAKA YA KIFEDHA


Ninayo furaha kuwasilisha Taarifa ya Mwaka na Matokeo ya Kifedha ya Benki ya CRDB na Kampuni zake Tanzu kwa Mwaka ulioishia Disemba 31, 2016.

Mwaka  2016 ulikuwa na umuhimu wa kipekee kwa Benki na Kampuni zake Tanzu kwani tuliadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Benki. Maadhimisho hayo yalienda sambamba na kutambua mchango wa wanahisa wetu, wateja na  wadau wengine.

 Pia Benki iliimarisha ahadi yake ya kuendelea kutoa huduma bora na za kipekee kwa miaka ijayo.
Mwaka 2016 ulikabiliwa na changamoto nyingi za kibiashara hasa utoaji wa mikopo kutokana na uamuzi wa serikali kuhamisha amana  za  mashirika ya umma kwenda Benki Kuu katika Akaunti ya Pamoja ya Hazina . 

Ili kukabiliana na mabadiliko hayo, Bodi ilitathmini upya sera na mikakati ya Benki na Kampuni zake Tanzu ili ziendane na hali halisi ya soko. Mojawapo ya mikakati hiyo ni kudhibiti  ukuaji wa rasilimali, mikopo na kuidhinisha mikopo ya ziada kutoka  taasisi za kimataifa kama vile European Investment Bank na  ICICI Bank kuziba pengo la mahitaji ya fedha na ukwasi.

Mikakati mingine iliyotekelezwa ni  kama ifuatavyo:
·             Kutathmini mfumo wa Usimamizi wa Vihatarishi na sera zake ili kuhakikisha kuwa usimamizi wa vihatarishi unakuwa sehemu ya usimamizi wa utendaji na mfumo wa malipo kwa wafanyakazi;
·             Kutathmini Sera ya Mikopo na ukomo wa kuidhinisha mikopo kwa    lengo la kupunguza  hatari ya mkopaji mmoja au sekta moja kuhodhi sehemu kubwa ya jumla ya mikopo;
·             Kuboresha utaratibu wa utoaji mikopo, ambapo inajumuisha mwanzo wa mkopo, tathmini, kuidhinisha, kufuatilia na kurejesha;
·             Kuimarisha usimamizi wa madeni/madai na kukusanya mikopo;
·             Kutathmini mifumo ya ndani ya usimamizi ili kuhakikisha inakuwa toshelevu na kuzingatiwa na wafanyakazi; na
·             Kuongeza ufanisi kiutendaji na kudhibiti gharama.
Hatua zilizotajwa hapo juu zilichukuliwa kutokana na kudorora kwa hali ya soko la kifedha –tatizo la ukwasi, kupanda kwa viwango vya riba na kutorejeshwa kwa mikopo kwa bidhaa zote. Uwiano wa mikopo iliyodorora uliendelea kuwa juu, kwa wastani wa asilimia 11 kwa mwaka mzima.

Tulianzisha vituo vidogo 61 vya kutoa huduma kwa msaada wa Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha nchini (FSDT) na Programu ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF). Hatua hii bila shaka itaongeza uwezo wetu wa kukusanya mapato kutoka makundi ya wafanyabiashara ndogo ndogo.

Matokeo ya Kifedha
Benki ya CRDB imeendelea kuwa imara katika soko, ikimiliki zaidi ya asilimia 20 ya jumla ya amana na rasilimali katika sekta ya benki, ambayo imeifanya ishike nafasi ya kwanza kwa ukubwa nchini  Tanzania. Kwa upande wa faida, tumeendelea kushika nafasi ya pili, ijapokuwa faida hiyo ilipungua hadi shilingi bilioni 74.1 kutoka shilingi bilioni 129.0 iliyopatikana mwaka uliopita. 

Jumla ya rasilimali za Benki ya CRDB na Kampuni zake Tanzu iliongezeka kwa asilimia  3 hadi shilingi bilioni 5,423.9  (kulinganisha na shilingi bilioni 5,407.8 mwaka 2015) na amana zilipungua kidogo kwa asilimia 3 hadi shilingi bilioni  4,113.8 ilipofika Disemba 31, 2016.

Mafanikio Muhimu ya Kimkakati
Matokeo chanya ya kampuni zetu tanzu ni mafanikio ya mkakati wa kupanua huduma zetu za kibenki na kiashiria cha mapato kuendelea kuongezeka miaka ijayo. Kwa mwaka husika, kampuni tanzu nyingine —CRDB Insurance Broker—ilianzishwa. Kampuni zote tanzu zilichangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Benki mwaka 2016.

Benki imeendelea  kuimarisha  ufanisi na uwezo wake kiutendaji  kwa kuboresha mfumo wake mkuu wa kutoa huduma za kibenki, kuongeza tija na kuzindua mfumo unaojiendesha wa maombi ya mkopo na taratibu za mikopo. Mfumo wa mawasiliano uliboreshwa kutoa huduma bora na zenye uhakika hasa katika mfumo wa kibenki wa kidijitali.

Kwa mara ya kwanza Benki ilitambuliwa na wakala wa kimataifa wa kutoa viwango vya ubora, Moody’s  kwa kupewa alama  B1, na kuifanya CRDB kuwa benki ya kwanza nchini Tanzania kufikia kiwango hicho. Haya ni mafanikio makubwa kwa Benki kwani inawahakikishia wawekezaji, wanahisa na wateja wetu kuwa Benki na Kampuni zake Tanzu zinafanya vizuri na zinaweza kukopeshwa.

Pamoja na sababu nyingine, kutambuliwa na wakala wa kimataifa wa kutoa viwango kuliisaidia Benki kupata fedha kiasi cha shilingi bilioni  85 kutoka taasisi mbalimbali za kifedha, ambazo ni pamoja na  Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Katika kipindi cha mwaka husika, Benki ilitunukiwa tuzo mbalimbali ambazo ni 8 Tuzo hizo ni ushahidi tosha kwa wateja wetu na wadau wengine kuhusu kukubalika na kuaminika kwa huduma za Benki na bidhaa zake na kutoa motisha kwa menejimenti na wafanyakazi.


Mabadiliko katika Bodi
Napenda kuwashukuru Wajumbe wa Bodi kwa kunichagua ili nihudumu katika Bodi ya Benki ya CRDB kama Mwenyekiti kuanzia mwezi Julai mwaka 2016. Naona fahari kuwatumikia katika nafasi hii na napenda kuwahakikishia wanahisa na wadau wengine kuwa nitajituma kwa nguvu zangu zote kwa ajili ya mafanikio ya Benki na Kampuni zake Tanzu.

Muda wa Mwenyekiti wa Bodi aliepita Bw. Martin Jonas Mmari (ambae aliteuliwa    na Mfuko wa Pensheni wa PPF), ulikwisha mwezi Julai mwaka 2016. Bw. Mmari alikuwa Mwenyekiti wa Bodi kwa muda mrefu na tutamkumbuka kwa uzoefu wake. Nachukua fursa hii kumshukuru kwa kujitolea kwa muda wote aliohudumu katika Bodi na namtakia mafanikio katika shughuli zake nyingine za kimaisha.

Nafasi ya Bw. Mmari ilijazwa na Bw. Hosea Ezekiel Kashimba ambae aliteuliwa na Mfuko wa PPF. Bw. Kashimba ana uzoefu katika masuala ya ukaguzi wa hesabu na fedha.

Wajumbe watatu wa Bodi ambao ni Bw. Boniface Charles Muhegi, Bw. Ally Hussein Laay na Bw. Adam H. Mayingu walistaafu kwenye Mkutano Mkuu  uliofanyika Mei 21, 2016. Bw. Mayingu aliamua kutogombea tena. Tutamkumbuka kwa mchango wake na nachukua nafasi hii kumtakia afya njema na mafanikio katika shughuli zake nyingine.  Bw. Boniface Charles Muhegi na  Bw. Ally Hussein Laay walichaguliwa kwa mara nyingine. 

Nampongeza Bw.  Muhegi kwa kuchaguliwa na wanahisa na pia nawashukuru kwa dhati wanahisa wenzangu kwa kunichagua tena katika nafasi hii.

Profesa Mohamed Hersi Warsame alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Bodi kuwakilisha kundi la wanahisa wenye kati ya asilimia 1 na 10 ya hisa za Benki. Bi. Madren N. Oluoch-Olunya alichaguliwa kuwa  Mjumbe Huru wa Bodi akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Lawrence N. Mafuru.  Tunahisi kupendelewa kuwa na Profesa  Warsame na Bi Oluoch-Olunya kwenye Bodi kutokana na uzoefu wao katika masuala ya fedha, sheria, utawala bora na rasilimali watu.

Kwa mara nyingine tena napenda kuwakaribisha Bw. Hosea Ezekiel Kashimba, Profesa Mohammed Hersi Warsame na Bi  Madren N. Oluoch-Olunya kwenye bodi.

Mapendekezo ya Gawio
Ninayo furaha kuwasilisha mapendekezo ya Bodi ya Gawio la shilingi 10 kwa kila hisa kwa mwaka ulioshia Disemba 31,  2016 litakalolipwa kwa wanahisa watakaokuwemo kwenye daftari hadi tarehe ……………  Azimio litawasilishwa kwenye Mkutano Mkuu wa 22 wa Benki ya CRDB  utakaofanyika Mei 20, 2017 ili kuidhinishwa na wanahisa.

Matarajio ya baadaye  
Mwaka 2017 unategemewa  kuwa na changamoto kutokana na kutotabirika kwa sera na ukuaji wa uchumi nchini na duniani kwa ujumla. Mabadiliko ya sera nchini Tanzania yanayojumuisha mabadiliko ya kiuchumi na kimuundo na mabadiliko ya mfumo wa usimamizi yanafanya mazingira ya biashara kutotabirika. 

Kutokana na hali hiyo, Bodi imechukua tahadhari katika kutekeleza mkakati wa Benki kwa mwaka 2017 -- Msukumo mkubwa ni kujiimarisha na kudhibiti vizuri gharama za uendeshaji – kwa kupunguza kasi ya kupanua mtandao na kuboresha matumizi ya rasilimali ili kuongeza mapato. Bodi itaendelea kuwa makini na kubadili mikakati kadri iwezekenavyo ili kukabiliana na mabadiliko yoyote ambayo yanaweza kuathiri uendeshaji au faida ya Benki.

Bodi inatarajia kuwa Benki na Kampuni zake Tanzu zitapata mafanikio mwaka 2017 na miaka ijayo na kulipa pato zuri zaidi kwa wanahisa wetu.

Shukrani
Nawashukuru wajumbe wote wa Bodi kwa imani yao na kumuunga mkono Mwenyekiti.  Natoa  shukrani za dhati kwa taasisi za usimamizi, wanahisa na wateja kwa kuendelea kuwa na imani na kuiunga mkono Benki kwa kipindi cha mwaka mzima.

Naishukuru menejimenti na wafanyakazi kwa kujituma, ubunifu na ushirikiano ambao umekuwa msingi wa mafanikio ya Benki katika kipindi ambacho kumekuwa na changamoto za kibiashara. Tuna kila sababu ya kujivunia kuwa na timu ya menejimenti na wafanyakazi wanaojituma na tunategemea mafanikio zaidi mwaka 2017.

Tunashukuru kwa ushirikiano mkubwa tuliopata kutoka serikali za Tanzania na Burundi kwa kipindi chote cha mwaka husika.

Kwa mara nyingine tena nachukua nafasi hii kuwatakia wateja wetu, wanahisa, menejimenti, wafanyakazi na wadau wetu wote heri na mafanikio kwa mwaka 2017!
Mr. Ally Hussein Laay
Mwenyekiti wa Bodi

 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Ally  Laay, akifafanua jambo kuhusu matokeo ya  kifedha kwa mwaka  2016 jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu wa Benki ya CRDB, John Rugambo. (Picha na Francis Dande).

 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Ally  Laay, akifafanua jambo kuhusu matokeo ya  kifedha kwa mwaka  2016 jijini Dar es Salaam. 

No comments:

Post a Comment

Pages