Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeutaarifu Umma juu ya kuendelea na taratibu za kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Mbunge wa Viti maalumu(CCM) Sophia Simba aliyefukuzwa uanachama wa Chama cha Mapindizi (CCM) Machi 11, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji(R) Semistocles Kaijage imeeleza kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemjulisha Mwenyekiti wa Tume kuwa kufuatia Mbunge huyo kufukuzwa uanachama wa CCM hivyo kiti cha Mbunge huyo kiko wazi.
Alisema kuwa Ibara ya 67(1) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inaeleza kuwa ili mtu ateuliwe au achaguliwe katika nafasi ya ubunge ni lazima awe mwanachama aliyependekezwa na Chama chake husika cha siasa.
“Kwa kuwa ndugu Sophia Mnyambi Simba amefukuzwa uanachama wa Chama kilichomdhamini, Ibara ya 67(2)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza kuwa mbunge huyo amepoteza sifa za kuteuliwa au kugombea Ubunge” alisema Jaji(R) Semistocles Kaijage.
Aliendelea kwa kusema kuwa kutokana na kuwepo kwa nafasi hiyo taratibu za kujaza nafasi hiyo zinaendelea kwa kuzingatia kifungu cha sheria 86(8) cha Sheria ya Uchaguzi Sura ya 343.
Kifungu hicho kinasema, orodha ya majina wanawake wagombea waliopendekezwa na tume kwa mujibu wa Ibara 78(4) ya Katiba na kila chama cha siasa kwa uchaguzi mkuu, kwa kuzingatia Ibara 76(3) ya Katiba, itakuwa orodha sawa na ile itakayotumiwa na tume kwa madhumuni ya kujaza nafasi yoyote iliyowazi katika ofisi ya mbunge wa viti maalum vya wanawake wakati wa kipindi kizima cha uwahi wa Bunge.
No comments:
Post a Comment