NA MWANDISHI
WETU
ZIKISALIA
siku sita kabla ya kishindo cha Tamasha la muziki wa injili la Pasaka
litakalofanyika katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, waimbaji wote
wapo katika maandalizi ya mwisho kabla ya tukio.
Tamasha hilo
la kimataifa litakalozinduliwa Uwanja wa Uhuru mbele ya mgeni rasmi Waziri wa
Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kwa niaba ya Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu
Hassan, litafika pia Simiyu na Mwanza.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana kuhusu maandalizi ya tukio hilo, Mwenyekiti wa Kamati
ya Maandalizi, Alex Msama alisema kila kitu kinakwenda vizuri na waimbaji wote
wapo katika maandalizi.
“Nashukuru
kwa upande wetu Kamati mipango inakwenda vizuri kama ilivyopangwa. Kama
unavyojua, Pasaka ilionekana kama vile iko mbali sana, lakini siku zimefika,”
alisema Msama.
Alisema anashukuru
pia waimbaji wote watakaohudumu katika tamsha la mwaka huu, wapo vizuri na
wanaendelea na maandalizi ya mwisho kuelekea kishindo cha Jumapili katika
Uwanja wa Uhuru.
Msama ametoa
wito kwa wadau wa muziki wa injili kulipokea tukio hilo kwa mikono miwili
kupata Baraka za Mungu kupitia tukio hilo lenye hadhi ya kimataifa
litakalowaleta waimbaji wa ndani na nje ya nchi.
Alisema kwa
kutambua kiu ya wengi kutaka kulishuhudia Tamasha hilo, ndio maana wameweka
viingilio vya kawaida kuanzia sh 10,000 kwa viti maalumu, sh 5000 kwa wakubwa
na watoto sh 3,000.
Msama
alisema baada ya kutoka Uwanja wa Uhuru, uhondo wa tukio hilo utahamia mkoa wa
Simiyu hapo April 22 na siku itakayofuata, itakuwa zamu ya wakazi wa jiji la
Mwanza katika Uwanja wa CCM Kirumba.
Waimbaji
ambao watapamba tukio hilo ni mwimbaji wa kimataifa wa Afrika Kusini, Solly
Mahlangu, Mercy Masika na Danny ‘M’ na Faustine Munishi kutoka Kenya.
Kwa upande
wa kwaya, ni Ulyankuru maarufu kama Kwa Viumbe Vyote, Kinondoni Revival Choir itakayozindua
kazi yao mpya isemayo ‘Ngome Zimeanguka’ na Vijana KKKT Tabata, jijini Dar es
Salaam.
Waimbaji ni
Rose Muhando atakayezindua albamu yake ya Jitenge na Ruth, Jesca BM, Upendo Kilahiro,
Matha Mwaipaja, Christina Shusho, John Lissu na Boniface Mwaitege.
No comments:
Post a Comment