Mwandishi Wetu, Tabora
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli leo ameagiza ujenzi wa mradi wa jengo la abiria 500 kwenye Kiwanja cha Ndege cha Tabora uanze mara moja.
Mhe. Rais ametoa kauli hiyo mara baada ya kufungua ujenzi wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Kiwanja cha Ndege cha Tabora, ambapo alisema sasa abiria wataongezeka kutokana na kukamilika kwa ujenzi huo, hivyo italazimu jengo kubwa lenye kuchukua abiria 500 kwani la sasa lenye uwezo wa kuchukua abiria 50 halitatosha.
“Ninaimani kubwa kwa ujenzi huu lazima idadi ya abiria itaongezeka zaidi hivyo kwa hili jengo dogo halitatosheleza abiria watakaoongezeka hivyo, namuagiza Waziri (Makame Mbarawa) kuanza mchakato wa ujenzi wa jengo hilo kubwa, ,” alisisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe . Rais amesema kutokana na ukarabati na upanuzi huo sasa kiwanja hichi kitaruhusu kutua kwa ndege kubwa zaidi za ndani na nje ya nchi, na kufanya wakazi wa mkoa wa Tabora kutumia uisafiri wa ndani kwa kwenda Dar es Salaam, Burundi, Kenya, Rwanda na maeneo mengine.
Amesema anarajia ujenzi huo utakamilika mapema zaidi na atakuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa jengo hilo, na ninawapongeza sana Wizara pamoja na wafanyakazi wote wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege Tanzania, kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Mhe. Rais amesema serikali yake inataka maendeleo ya kuwa na viwanja vya ndege vya uhakika, barabara na maji na sio siasa, ambazo hazina tija kwa maisha yao ya sasa na baadaye.
“Mimi ni Rais wa Watanzania wote na sio wa CCM pekee na ndio maana ninachochea maendeleo tena ya haraka ambayo yatafanikisha wananchi kuwa na maisha mazuri ikiwa ni pamoja na kuitumia miundombinu katika biashara na maisha yao ya kila siku,” amesema Mhe. Rais.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais ametaka barabara ya kutua na kuruka kwa ndege irefushwe zaidi ili kuruhusu ndege kubwa kutua kwa wingi.
Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa amesema sambamba na maboresho hayo ya miundombinu katika kiwanja cha ndege cha Tabora, sasa ujenzi wa jengo jipya la abiria unatarajia kuanza mara moja kwa ufadhili wa fedha za mkopo kutoka Benki ya Uwekezaji ya Uaya (European Investment Bank-EIB), na litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 500,000 kwa mwaka.
Pia Mhe. Prof. Mbarawa amesema mradi huu wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Kiwanja cha Ndege cha Tabora umegharamiwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia.
Mhe. Prof. Mbarawa amesema mradi huu umejumuisha barabara za kuruka na kutua ndege, barabara ya kiungio, maegesho ya ndege, taa na mitambo ya kiusalama ya kuongoza ndege wakati wowote na kituo cha umeme.
“Kiwanja sasa kimeongezewa uwezo wa kutoa huduma kwa saa 24, na vilevile maboresho yanayofanyika katika viwanja viwanja vya ndege yanalengo la kuvutia ujaji wa mashirika mengi zaidi ya ndege pamoa na kuongeza uwezo wa kuhudumia ndege nyingi zaidi, na sasa serikali inadhamiria ya kununua ndege nne na jum;a itafanya idadi ya ndege sita,” amesema Mhe. Prof. Mbarawa.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kiwanja cha Ndege Tanzania (TAA), Bw. Salim Msangi amesema ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya kiwanja cha ndege cha Tabora umefanyika kwa awamu tatu, ambapo ni kujenga barabara ya kwanza ya kuruka na kutua kwa ndege kwa kiwango cha lami kwa urefu wa mita 1900 na upana wa mita 30.
Bw. Msangi amesema awamu ya pili ilihusisha ujenzi wa barabara ya pili ya kuruka na kutua kwa ndege kwa kiwango cha lami yenye urefu wa mita 1260 na upana wa mita 23; maegesho ya ndege yenye uwezo wa kuegesha ndege tatu zenye ukubwa wa ATR 72 au Bombardier dash 8 Q400 kwa wakati mmoja; kujenga kiungio yenye urefu wa mita 250; usimikaji wa taa na mitambo ya kuongezea ndege wakati wa kutua na kuruka.
“Hii awamu ya pili ilihusisha vitu vingi ikiwepo pia ujenzi wa kituo cha kufua umeme na usimikaji wa jenereta lenye kVA 500; ujenzi wa uzio wa usalama wa urefuwa kilometa 2.6 na ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua,” amesema Bw. Msangi.
Bw. Msangi amesema awamu ya tatu itahusisha ujenzi wa jengo jipya la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 500,000 kwa mwaka; ujenzi wa barabara ya kuingia kiwanjani na eneo la maegesho ya magari, ambapo kwa ujumla utafadhiliwa na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya na utagharimu shilingi za Kitanzania Bilioni 27.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli akiwasili kwenye kiwanja cha Ndege cha Tabora tayari kwa uzinduzi wa mradi wa ujenzi ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya kiwanja hicho.
Mhandisi Neema Joseph (kulia) akimpa taarifa Mhe Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli za ujenzi wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Kiwanja cha ndege cha Tabora.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege Tanzania (TAA), Bw. Salim Msangi (kulia mwenye tai nyekundu) akiongozana na viongozi wengine wa serikali kumsindikiza Mhe. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli baada ya kufungua ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Tabora. DSC_9451:
Mhe Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli akiongozana na msafara wake kwenda kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Kiwanja cha Ndege cha Tabora leo.
Rais Mhe. Dk. John Pombe Magufuli akipeana mikono na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Kiwanja cha Ndege cha Tabora.
No comments:
Post a Comment