WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasihi Watanzania wanaofanya kazi
katika viwanda mbalimbali nchini kufanya kazi kwa bidii na kuwa waaminifu.
Amesema Tanzania imedhamiria kukuza uchumi wake kupitia sekta ya
viwanda hivyo ni vema watakaopata fursa ya ajira katika viwanda hivyo kuwa waadilifu.
Ameyasema hayo leo (Jumapili, Julai 30, 2017) wakati akizungumza
na wafanyakazi wa kiwanda cha gesi cha Ikama kilichoko wilayani Rungwe.
Waziri Mkuu amesema wakati Serikali
ikiendelea kuwakaribisha wawekezaji nchini, wananchi walioajiriwa kwenye maeneo
hayo wawe waaminifu.
“Mnatakiwa muwe waaminifu, msibebe kitu chochote ndani ya
kiwanda bila ya ridhaa ya wamiliki kwa kuwa mtaonyesha taswira mbaya kwa
wawekezaji.”
Amesema uaminifu wao ndio utawezesha Watanzania wengi kupata
ajira kwenye viwanda hivyo ambavyo vimejengwa katika maeneo yao.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi
ya Wakurugenzi wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na kampuni ya TOL Gases,
Mhandisi Harold Temu alisema kiwanda
kinauwezo wa kuzalisha tani 46 kwa siku.
Alisema gesi inayozalishwa kiwandani hapo ni ya Carbon Dioxide
ambayo inauzwa nchini na nchi jirani za Zambia, Malawi, Zimbabwe na Congo.
Mhandisi Temu alisema wateja wakubwa wa gesi hiyo ni viwanda vya
kutengenezea soda, bia na pia hutumika katika kuhifadhia chakula na kwenye
vifaa vya kuzimia moto.
Mapema Waziri Mkuu
alitembelea kiwanda cha kuchakata majani ya chai cha Katumba, ambapo alisema Serikali
inaimarisha Ushirika wa zao hili ili wakulima waweze kupata tija.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 30, 2017
No comments:
Post a Comment