*Ameonya zisitumike kuvushia wahamiaji haramu na dawa
za kulevya
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amezindua meli mbili za mizigo za Mv Njombe na Mv Ruvuma zitakazotumika
katika kusafirishia mizigo kwenye ziwa Nyasa na kuonya kwamba zisitumike kama
eneo la kuvushia wahamiaji haramu na dawa za kulevya.
Amesema
kukamilika kwa ujenzi wa meli hizo zilizogharimu sh. bilioni 11.253 ni utekelezaji
wa ahadi ya Rais Dkt. John Magufuli alizozitoa katika ilani ya uchaguzi ya CCM ya
mwaka 2015-2020 kwa lengo la kutatua
changamoto ya usafiri wa abiria na mizigo katika ziwa Nyasa.
Amesema
ni jambo la faraja na la kujivunia kwa Serikali na wananchi kwa pamoja kushuhudia
meli zilizotengenezwa na Mtanzania, zikiwa zimekamilika tayari kwa kuanza kazi
ya kuwahudumia wananchi, ambapo awali suala hilo lilikuwa likifanywa na raia wa
kigeni.
Waziri
Mkuu amezindua meli hizo zilizojengwa na kampuni ya Kitanzania ya M/S Songoro Marine Transport leo (Jumamosi, Julai 29,
2017) katika bandari ya Kiwira wilayani Kyela akiwa katika ziara yake ya kikazi
mkoani Mbeya.
Amesisitiza
kwamba meli hizo zitumike katika kukuza uchumi wa wananchi kwa kusafirisha
mizigo na biashara halali kati ya nchi za Tanzania na Malawi na zisitumike kama
eneo la kuingiza wahamiaji haramu pamoja na dawa za kulevya nchini.
Waziri
Mkuu amewataka wananchi wa maeneo hayo kuwa walinzi na kuhakikisha meli hizo
zifanya shughuli halali za kiuchumi ambazo zitawaletea tija wao na Taifa kwa
ujumla na kamwe wasikubali zikatumika kama kichaka cha uhalifu.
“Changamoto
ya usafiri wa mizigo katika ziwa Nyasa itakuwa historia kwani meli hizi
zitarahisisha usafiri na kupanua wigo wa biashara kati ya Tanzania nan chi za
Malawi na Msumbiji, hivyo tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa kutoa
ahadi hii ambayo leo utekelezaji wake umekamilika.”
Awali,Naibu
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) anayeshughulikia Miundombinu,
Mhandisi Karim Mataka alisema ujenzi wa meli hizo ulianza Juni 2015 zina uwezo
wa kubeba tani 1,000 za mizigo kwa kila moja.
Mhandisi
huyo alisema mbali na kukamilika kwa mradi huo pia TPA imeingia mkataba na
kampuni ya M/S Songoro Marine Transport Ltd kwa ajili ya ujenzi wa meli ya
abiria yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 300 za mizigo. Mradi huo ambao
upo katika hatua za mwisho kamilika utagharimu sh. bilioni 9.12.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI,
JULAI 29, 2017
No comments:
Post a Comment