HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 02, 2017

LISHE DUNI: Kichocheo cha watoto kufeli mitihani

NA HAPPINESS MNALE

FEBRUARI 18, 2013 ni siku ambayo iliingia katika kumbukumbu za historia ya elimu nchini Tanzania, pale taifa liliposhuhudia kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012 yakionyesha kuwa zaidi ya nusu (asilimia 50) ya watahiniwa wa kidato cha nne walikuwa wamefeli kwa kupata sifuri.

Katika matokeo hayo wanafunzi 240,903 (sawa na asilimia 61) ya 397,126 waliofanya mtihani wa kidato cha nne 2012 walikuwa. Katika matokeo hayo ni asilimia 34 walipata daraja la IV (division four), ikimaanisha kwamba ni asilimia sita pekee waliopata daraja la I, II na III kwa ujumla wao.

Kilio kilisikika kutoka pande zote za nchi, mijini na vijijini. Ni wakati huo ambao tulishuhudia aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Profesa Joyce Ndalichako akingoka katika taasisi hiyo. Msomi huyo hivi sasa ndiye waziri mwenye dhamana ya elimu akiwa mteule wa Rais John Magufuli.

Matokeo hayo yaliyotajwa kuwa janga la kitaifa yalimsukuma Waziri Mkuu wa wakati huo, Mizengo Pinda, kuunda tume kuchunguza kilichosababisha matokeo mabaya na kutoa mapendekezo kuhusu nini kifanyike.

Tume hiyo iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wake, Profesa Sifuni Mchome na wajumbe 13 ilifanya kazi yake na kurejea na majawabu na mapendekezo mengi. Ripoti ya tume hiyo ilishabihiana na ripoti nyingi ndogo zilizokuwa zimetolewa na taasisi za kijamii, mashirika yasiyo ya kiserikali na vyama vya kitaaluma.

Kwa ujumla sababu zilizotajwa ziligusa maeneo kama sera, mfumo wa elimu nchini, utendaji kwa maana ufundishaji na mazingira ya kujifunzia, rasilimali kama vile fedha, maslahi ya walimu na sababu nyinginezo.

Hata hivyo lipo eneo ambalo tatifi hizo hazikuligusa licha ya kwamba limekuwa likitajwa katika nyaraka nyingine za serikali ambazo hazigusi moja kwa moja mfumo wa elimu. Hili si jingine bali ni suala la lishe.

Lishe haikutajwa, haikuwahi kutajwa na hakuna hakika kama itakuja kutajwa kuwa miongoni mwa visababishi vya wananfunzi wawe wa shule za msingi au za sekondari kufeli masomo yao.

Lakini ukweli ni kwamba tafiti za wataalamu zinathibitisha kwamba kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya lishe na uwezo wa kiakili wa mtu. Kwa maana hiyo, ukosefu wa lishe bora unaweza kuwa miongoni mwa sababu za watoto walipo shule kufanya vibaya.

Dk. Marsha Maccata ambaye ni mfamasia anasema uwezo wa kiakili hujengwa tangu mtoto akiwa tumboni mwa mama yake na kwamba ujenzi huo hutokana na vyakula ambavyo mama mjamzito anavitumia katika kipindi hicho,

“Katika masuala ya lishe kuna kitu kinaitwa siku 1,000; hizi ni siku tangu mimba inapotungwa, ikakua, mtoto kuzaliwa na kulelewa hadi anapofikisha umri wa miaka miwili.

“Ni kipindi muhimu sana cha kuhakikisha kwamba kwanza mama anapata lishe yenye virutubisho vyote na baada ya kujifungua mtoto naye anakuzwa akizingatia vyakula vinavyostahili,”alisema Dk. Maccata.

Kauli yake inaungwa mkono na mtaalamu mwingine wa masuala ya wanawake, watoto na lishe katika hospitali ya Vijibweni, Kigamboni jijini Dar es Salaam, Dk. Fredy Mchinamnamba ambaye anasema ili mtoto kwa maana ya wananfunzi wanaosoma wafaulu vizuri shuleni, lazima wawe na msingi imara wa lishe bora tangu mimba inapotungwa.

Dk. Mchinamnamba anasema mtoto hawezi kukua na kustawi vema asipopata vitamini na madini muhimu na kwamba madhara yatokanayo na ukosefu wa lishe bora huonekana baadaye.

Lishe bora ni nini?

Lishe bora ni hali ya mwili kupokea chakula chenye virutubisho vyote muhimu kwa ajili ya kujenga, kukinga, kuupa mwili joto ili kuwezesha kufanya kazi vizuri.

Virutubisho hivyo ni pamoja na protini, wanga, vitamini, madini, nyuzi nyuzi na maji. Dk. Mchinamnamba anasema kwamba lishe bora huanza tangu mtoto anapokuwa tumboni mwa mama yake.

Dk. Mchinamnamba naye anasisitiza umuhimu wa kuzingatiwa kwa lishe bora kwa siku 1,000 za uhai wa mtoto, tangu pale anapotungwa mimba hadi mtoto anapotimiza miaka miwili.

Anasema kwa wazazi ni muhimu kuzingatia lishe bora katika siku hizo 1,000 kwa kuwa matokeo yake huendelea kwa kipindi chote cha maisha ya mwanadamu.

“Unajua umuhimu wa siku hizi huokoa vifo vya watoto zaidi ya 1,000,000 kwa mwaka duniani na zinaongeza kiwango cha kuelewa cha mtoto na kumwezesha kufanya vizuri shuleni na maishani yake yote kwa ujumala,”anasema daktari huyo.

Dk. Mchinamnamba anaendelea kusema kwamba mtoto akikosa lishe bora katika hizo siku 1,000 mara nyingi hupata udumavu ambao ni hali ya ubongo wake kutokua katika kiwango kinachotakiwa.

“Ukosefu wa lishe bora mwanzoni wakati wa utotoni huwasababishia udumavu wa kimwili, kushambuliwa na magonjwa mara kwa mara, matatizo ya kujifunza ambayo hudumu katika maisha yao yote,”anasema Dk. Mchinamnamba.

Anasema kwamba mtoto asipojengwa na lishe bora pindi mimba yake inapotarajiwa kutungwa na katika makuzi yake akiwa tumboni, anapozaliwa hadi miaka miwili lazima mfumo wa maisha yake hata atakapo kuwa mtu mzima uende ndivyo sinyo.

“Unajua ili tupate viongozi bora, wahandisi, walimu hata wanafunzi wenye uwezo ni lazima wajengwe katika katika lishe bora bila hivyo hawezi kukua, kustawi vema hasa asipopata vitamini na madini muhimu,akiwa mdogo,”

“Hapo unaweza kuona kwamba mambo mengine yanayotokea katika jamii ni madhara ya ukosefu wa lishe, mfano kuwa na viongozi ambao hata akizungumza wananchi wanajiuliza wana matatizo gani, wanafunzi wasioelewa darasani ama kufeli kwao tafiti zinaonyesha ni kutokana na udumavu ambao usababishwa na utapiamlo,”anasema.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira, January Makamba, aliwahi kuandika kwamba asilimia 42 ya watoto Tanzania wana udumavu kwasababu ya matatizo ya lishe na kuongeza: “Udumavu unapunguza upokeaji wa maarifa shuleni. Lishe muhimu kwa elimu”.

Mwalimu wa shule ya Msingi Mloganzila jijini Dar es Salaam, Maria Mpunga, anasema lishe ni muhimu kwani isipozingatiwa watoto hudumaa na kuwa wagumu kuelewa.

“Unakuta wakati mwingine tunafundisha na hata kurudia lakini mtoto haelewi, sasa unajiuliza ni njaa ama kitu gani, mimi naamini tunapaswa kuishi kwa kufuata vyakula ambavyo vitatupa lishe bora, hii itasaidia kuwajenga wanafunzi tunaowafundisha kuelewa kwa haraka.

“Elimu hii pia lazima ianzie shuleni, mimi huwa nawafundisha watoto kwamba lazima wale chakula chenye protini, wanga na vitamini, ninawafundisha kwa vitendo lengo ni kuondoa matatizo yatokanayo na lishe na udumavu,”anasema Mwalimu Mpunga.

Hali ilivyo nchini

Takwimu za iliyokuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zilizotolewa bungeni Aprili 2015 zinaonyesha kuwa zadi ya watoto 2.7 nchini wamedumaa, huku 446,000 kiwa na tatizo la ukondefu na 106,000 wanakabiliwa na utapiamlo mkali.

Licha ya kwamba hali ya udumavu nchini kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano imepungua kutoka asilimia 42 mwaka 201o hadi asilimia 34 miaka miwili iliyopita, kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa lishe na chakula nchini wa 2014, hali bado ni mbaya katika baadhi ya mikoa.

Mwaka jana aliyekuwa Waziri wa Afya, Dk. Seif Rashid aliliambia Bunge kuwa viwango vya udumavu katika mikoa tisa ni vya juu ikilinganishwa na igezo vya Shirika la Afya Duniani. Mikoa hiyo na viwango vyake vya asilimia kwenye mabano ni Kagera (52), Njombe (52), Iringa (51), Ruvuma (49), Kigoma (49), Rukwa (48), Geita (46),Dodoma (45) na Katavi (43).

Tukirejea mwaka 1996 hali ya utapiamlo mkali na udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano nchini ilikuwa ni asilimia 50 na miaka kumi baadaye (2005) ilikuwa asilimia 44.

Kwa maana hiyo tangu wakati huo hadi 2010 (miaka mitano) matatizo hayo yalipungua kwa asilimia 2 tu, huku ikikadiriwa kuwa wakati huo zaidi ya watoto milioni 3 wenye umri huo uliotajwa walikuwa wameathiriwa na matatizo hayo.

Mtaalamu wa lishe katika Taasisi ya Chakula na Lishe nchini, (TFNC) Mary Kabona, anasema licha ya kwamba takwimu zinaonyesha kushuka kwa udumavu na utapiamlo kutoka asilimia 42 mwaka 2010 hadi asilimia 34.7 mwaka 2014 bado hali hairidhishi katika baadhi ya mikoa.

Kabona anasema baadhi ya mikoa yenye tatizo hilo ina chakula cha kutosha na kwamba tatizo kubwa ni ulishaji wa watoto usiozingatia kanuni na taratibu za afya tangu mimba inapotungwa hadi kuzaliwa kwao.

Matokeo ya 2012

Wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mwaka 2012 ni dhahiri kwamba waliingia kidato cha kwanza 2009, wakiwa wamemaliza darasa la saba 2008 na walianza darasa la kwanza 2002 wakiwa na umri wa miaka kati ya 6 na 8.

Kama hivyo ndivyo, wengi wa watoto hao ni wale waliozaliwa kati ya mwaka 1994 na 1996 wakati tatizo la utapiamlo na udumavu nchini likiwa ni zaidi ya asilimia 50. Na kwa mikoa mingine kama takwimu zinavyoonyesha tatizo hilo lilikuwa kubwa zaidi.
Kwa maelezo ya wataalamu na madaktari ni dhahiri kwamba matokeo mabaya ya kidato cha nne ya mwaka 2012 kuna uwezekano mkubwa kwamba yalichangiwa na hali hii ya udumavu, matatizo yanayotoka na kukosa lishe bora walipokuwa watoto.

Taarifa za NECTA zinaonyesha kuwa miongoni mwa shule zilizofanya vibaya katika matokeo ya mtihani huo ni pamoja na zile zilizoko katika mikoa ya Kagera (Katoke Lweru), Ndame Sekondari (Unguja), pamoja na Kwamndolwa, Nkumba na Tongoni za Mkoa wa Tanga.

Kwa upande wa Lindi ambayo ina asilimia 54 kwa takimu za mwaka 2014 zilizotolewa na Wizara ya Afya, shule ya Mibuyuni ilikuwa mojawapo ya zilizofanya vibaya katika matokeo hayo ya mwaka 2012.

mnaleh@yahoo.com

No comments:

Post a Comment

Pages