Mkuu wa Mkoa wa Rukwa KamishnMstaafu Zelote Stephen
ameishauri kamati ya maandalizi ya nanenane nyanda za juu kusini kufikiria
kushirikisha nchi za SADC ili kuongeza hamasa na kuleta ushindani kwa
watanzania wafahamu yanayofanyika katika nchi za jirani.
Ametoa ushauri alipokuwa akifanya majumuisho baada ya
kutembelea mabanda 16 ya bidhaa mbalimbali za kilimo katika maonesho ya nane nane
kwa kanda ya nyanda za juu kusini yanayofanyika katika viwanja vya John
Mwakangale jijini Mbeya ambapo Mh. Zelote Stephen alikuwa mgeni rasmi wa siku
ya tatu tangu ufunguzi wa maonesho hayo.
“Tuachane na mazoea, maonyesho haya yana miaka 25 sasa tuyaboreshe
zaidi, isiswe ni mikoa hii tu saba, tupanue wigo, kwakiwa huku ni nyanda za juu
kusini basi tufikirie kuzishirikisha nchi za SADC ambazo zitasaidia kubadilishana
biashara na teknolojia pamoja na kutafuta masoko,” Alifafanua.
Akisisitiza suala hilo Mh. Zelote alibainisha kuwa nchi ya
Tanzania inafikika kwa njia zote, ardhini, majini na angani huku akitaja meli
mbili zilizozinduliwa Mkoani Mbeya na Waziri Mkuu Mh. Kasim Majaliwa, treni ya
TAZARA pamoja na ndege zinazomilikiwa na nchi yetu.
Aidha amezishauri halmashauri kuanza maandalizi kwa kuwa na
siku maalum kwaajili ya maadhimisho hayo kihalmashauri ili kuwapa ujuzi na
kujua ubora wa vitu ambavyo vinaweza kupelekwa kwenye maadhimisho ya nanenane
kikanda ili kuimarisha ushindani na kumpa kila mwananchi nafasi ya kuelimika
ili kuwa na kilimo chenye tija.
Akiunga Mkono Kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Mh. Kilolo Ntila alityekuwemo katika
msafara huo alisisitiza kuwa maonesho ya nanenane yanayofanyika kikanda yanalenga
watu wenye kipato cha kutoka katika halmashauri zao na kukusanyika jijini Mbeya
huku wakulima wasio na uwezo wakikosa elimu inayopatikana kutokana na maonyesho
hayo.
“Nikiongezea aliyoyasema Mheshimiwa Mkuu wangu wa Mkoa, kwa
nafasi yake namuomba aweze kushawishi haya makampuni makubwa kuweza kusambaza
wataalamu wao katika Halmashauri zetu ambapo kuna uhitaji mkubwa wa elimu hii
inayotolewa hapa katika viwanja hivi vya nanenane na wao ndio walengwa wakubwa
wa shughuli hii,” alisema.
Pamoja na hayo Mh. Zelote alitoa wito kwa wananchi wote
wenye nafasi wajitokeze kwa wingi kwenye maonyesho hayo ili waweze kuelimika
kutokana na mafunzo mbalimbali yanayotolewa viwanja hivyo vya nanenane na
kusifu maandalizi ya sherehe hizo.
No comments:
Post a Comment