WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuanzia sasa ni
marufuku kuweka bei ya tumbaku kwa dola za Marekani kwa sababu imechangia kuwaumiza
wakulima wa zao hilo.
Amesema wanunuzi wa zao hilo wana uhuru wa kuweka
bei zao kwa dola lakini bei hiyo itafsiriwe kwa shilingi za Kitanzania ili
wakulima waweze kutambua bei elekezi tangu mwanzo wa msimu.
Ametoa kauli hiyo leo jioni (Jumatano, Agosti 9,
2017) wakati akizungumza na wadau wa zao la tumbaku zaidi ya 600 wakiwemo wabunge,
viongozi wa dini, chama na Serikali kwenye mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa
Isike-Mwanakiyungi, mjini Tabora.
Hivi sasa bei elekezi kwa msimu huu wa tumbaku ni dola
mbili za Marekani kwa kilo moja ya tumbaku sawa na sh. 4,400 hadi sh. 4,500 za
Tanzania.
Hata hivyo, Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya
kwanza ya ziara yake mkoani hapa, alionya juu ya mkanganyiko unaowapata
wakulima na viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS) kwenye kutafsiri bei ya zao
hilo kutoka dola za Marekani.
“Kwa mfano, mkulima anapouza tumbaku anaambiwa kilo
zake zina thamani ya dola za marekani 90. Wakati anapokuja kulipwa bei ya
shilingi inakuwa imebadilika, kwa hiyo kama aliuziwa wakati thamani ya dola moja
ikiwa ni sh. 1,500/- na wakati wa kulipwa imefikia sh. 2,000/- hatalipwa kwa
bei ya sasa. Bali atalipwa kwa bei ileile ya zamani jambo ambalo linamuumiza
mkulima,” amesema.
Akiwa hapohapo ukumbini, Waziri Mkuu aliwauliza
wawakilishi wa benki za CRDB na NMB bei ya dola moja ni sawa na shilingi ngapi kwa
hapo Tabora, alijibiwa kwamba katika benki ya CRDB, dola moja ya Marekani
inauzwa kwa sh. 2,200 ilhali katika benki ya NMB, dola moja inauzwa kwa sh. 2,167.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, AGOSTI 9, 2017.
No comments:
Post a Comment