WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakuu
wa mikoa 11 inayolima pamba nchini wahakikishe wanasimamia vizuri wakulima wa zao hilo ili kuongeza uzalishaji na
kuwaletea tija wananchi.
Agizo hilo limetolewa leo (Jumanne, Septemba 26, 2017) na Waziri Mkuu wakati akizungumza na wakuu hao wa
mikoa kwenye kikao alichokitiisha mjini Dar es Salaam kujadili maendeleo ya zao
hilo.
Kikao hicho ni muendelezo wa kikao alichokitiisha mjini Dodoma (Ijumaa, Septemba 8, 2017) kujadili mbinu za
kufufua zao hilo.
Wakuu wa mikoa walioitwa kwenye kikao hicho ni kutoka mikoa ya
Shinyanga, Singida, Kagera, Tabora, Morogoro, Mara, Mwanza, Simiyu, Katavi,
Kigoma na Geita.
Waziri Mkuu amesema katika kipindi hiki ambacho msimu wa maandalizi
ya kilimo cha pamba umeanza ni vema kwa Maofisa Kilimo na Wagani wakawasimamia
wakulima kwa ukaribu ili wahakikishe wanafuata mbinu bora za kilimo.
Amesema iwapo wakulima watapata usimamizi mzuri kutoka kwa Maofisa
Ugani waliopo kwenye maeneo yao kuanzia hatua za awali za utayarishaji wa mashamba
yao itawasaidia katika kuongeza tija,
kwenye uzalishaji wao.
“Serikali inawataka Maofisa Kilimo na Wagani wawasimamie
wakulima kuanzia maandalizi ya shamba, kupanda, matumizi ya pembejeo na dawa,
kuvuna na kutafuta masoko ili kilimo cha zao hilo kiweze kuwaongezea tija.”
Amesema Maafisa Kilimo wote walioko kwenye kila Halmashauri ni
lazima wahusike kikamilifu katika kuwaelekeza wakulima namna ya kutumia mbinu
bora za kilimo ili waweze kupata mazao mengi , hivyo kujikwamua kiuchumi.
Pia Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Vyuo vya Kilimo nchini wahakikisha
wanakuwa na mashamba darasa yatakayotumika na wakulima na wanafunzi wao kujifunza
mbinu bora za kilimo kwa vitendo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na
Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba; Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI; Bw.
Suleiman Jafo, Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo,
Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Tito Haule na Mkurugenzi Uhamasishaji
Mazao, Bw. Twahir Nzallawahe.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, SEPTEMBA 26, 2017.
No comments:
Post a Comment