HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 14, 2017

Rais Magufuli: Hatutaufuta Mwenge wa Uhuru

Na: Fatma Salum (MAELEZO)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia watanzania kuwa hana mpango wa kufuta mbio za mwenge wa uhuru kutokana na madai ya baadhi ya watu wanaosema kwamba hauna faida.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Mjini Zanzibar alipokuwa akihutubia kwenye sherehe za kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru zilizofanyika kwenye uwanja wa Amani ikiwa ni siku ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

“Mwenge wa Uhuru hatutaufuta kwa sababu unachochea maendeleo, katika kipindi cha uongozi wangu na Dkt. Shein Mwenge utaendelea kukimbizwa nchini kote,” alisisitiza Rais Magufuli.

Alisema kuwa baadhi ya watu wanaodai kwamba mwenge huo unaleta hasara kutokana na gharama zinazotumika, wazingatie kuwa bajeti ya kukimbiza mwenge ni ndogo ukilinganisha na faida kubwa inayopatikana kupitia miradi inayotekelezwa kutokana na hamasa ya mbio za mwenge kwenye maeneo mbalimbali kote nchini.

Aidha alibainisha kuwa mwenge wa uhuru ni moja ya tunu za nchi ya Tanzania na alama ya uhuru na utaifa wetu hivyo kuufuta ni sawa na kufuta alama kubwa inayotambulisha nchi yetu.

“Mwenge huu unatuunganisha watanzania na kuimarisha muungano wetu na yeyote atakayejaribu kuharibu amani au kuvuruga muungano tutapambana naye,” alisema Rais Magufuli.


Akizungumzia kuhusu kumbukumbu ya kifo cha Mwl. Nyerere, Rais Magufuli alisema kuwa ni jukumu la kila mtanzania kuyaenzi kwa vitendo mambo yote mazuri yaliyoachwa na muasisi huyo wa taifa letu ili tuweze kuwa na Tanzania yenye maendeleo.

Alisema kuwa Mwl. Nyerere ameacha mengi mazuri hivyo ni mfano wa kuigwa katika nchi yetu kwa sababu alikuwa ni mzalendo, mpigania uhuru, mpenda amani, haki na usawa kwa wote.

“Serikali zote mbili zimejipanga kuyasimamia na kuyatekeleza mambo yote mazuri yaliyoachwa na waasisi wa nchi hii Mwl. Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume kwa kuwa uzalendo wao na mapenzi mema kwa taifa letu vimeweza kutufikisha hapa tulipo,” alisema Rais Magufuli.

Akizungumzia mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika Serikali ya Awamu ya Tano Rais Magufuli alisema kuwa baada ya Serikali kuchukua hatua za kudhibiti sekta ya madini uzalishaji umeongezeka ikiwemo almasi na tanzanite.

Aidha alibainisha kuwa kwa mujibu wa taarifa ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), mwaka 2017 miradi 271 ya uwekezaji imeanzishwa yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.4.

Alisema kuwa ana uhakika Tanzania itafanikiwa kufikia uchumi wa kati kwa kuwa viwanda vingi vinaendelea kujengwa na Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ili tuweze kufika tunapokusudia.

Akitoa taarifa kwa Mgeni Rasmi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama alisema kuwa miradi 151 yenye thamani ya shilingi bilioni 569.8 imezinduliwa na mbio za mwenge kwenye Halmashauri na Mikoa mbalimbali nchini.

Aidha alieleza kuwa miradi 21 yenye thamani ya shilingi bilioni 3.1 ilibainika kuwa na kasoro ikiwemo ubadhirifu wa fedha za umma hivyo haikuzinduliwa.
Mbio za Mwenge wa uhuru zilizinduliwa mapema mwaka huu mkoani Katavi na kilele chake kimefanyika Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

Pages