Singida, Tanzania
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Iramba Emmanuel
Luhahula, asimamie kuvunjwa kwa bodi ya Ushirika wa Kijiji cha Msai Wilayani
Iramba ndani ya wiki mbili, kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya shilingi
milioni 50.
Dkt Nchimbi ametoa
agizo hilo mwishoni mwa wiki alipokuwa katika mkutano na wakulima wa Pamba wa
Kijiji cha Msai, ambao wamemueleza kutokuwa na imani na viongozi wa bodi hiyo
kutokana na upotevu wa fedha hizo na wakiwa hawajachukuliwa hatua yoyote.
Wakulima hao
wamemueleza Mkuu wa Mkoa kuwa fedha zaidi ya milioni 50 zilitolewa na seikali
kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la ghala la ushirika wa kijijini hapo lakini
hakukuwa na ujenzi wowote uliofanyika huku wakifuatilia hawapewi majibu sahihi.
Wamesema wana
ushirika walijitahidi kutuma mwenyekiti wa Kijiji hicho kufuatilia upotevu huo
bila mafanikio jambo lililowakatisha tamaa ya kuendelea na ushirika.
Dkt Nchimbi amesema “moja
ya Muhimili wa mafanikio ya kilimo cha pamba ni ushirika ulio imara, tunakoelekea
kwenye kilimo cha pamba chenye tija hawa wasiowaaminifu kwenye bodi watatukwaza
na kutukwamishwa, kama bodi haifanyi kazi vizuri kwanini iendelee?, Mkuu wa
Wilaya naimani kwa utendaji wako mzuri hili halitachukua zaidi ya wiki mbili”.
Aidha amemtaka Afisa
Ushirika Mkoa wa Singida kusimamia na kutoa ushauri wa kitaalamu wakati wa
kuvunjwa kwa bodi hiyo kwakuwa kazi ya mkoa ni kusuluhisha sio kutafuta maelezo
marefu huku wananchi wanapotezewa muda.
“Afisa Ushirika
hakikisha tarehe ishirini mwezi huu bodi hiyo iwe imeivunjwe na kuundwa bodi
mpya ambayo itasimamia ushirika kwa umakini ili kuinua kilimo cha pamba Iramba”,
amesisitiza Dkt Nchimbi.
Aidha Dkt Nchimbi amewatoa
hofu wakulima kwakuwa mbegu aina ya UKM 08 za manyoya pamoja na viuatilifu zitafika
na kusambazwa kwa wakati huku akiwataka kupanda kitaalamu ili kwa ekari moja iwe
na miche elfu 22 na mkulima avune zaidi ya kilo elfu moja za pamba.
Pia amewaagiza
maafisa ugani wote kulima pamba ili mashamba yao yawe mashamba darasa, huku
wakitakiwa kuhakikisha hakuna makosa katika hatua yoyote kuanzia kwenye kuandaa
mashamba, kupanda na kwenye upuliziaji dawa, bila kusahau kutoa taarifa kwa
wananchi katika kila hatua.
Dkt Nchimbi amewapa
wakulima wawili hodari wa zao la pamba zawadi ya kilo tano kwa kila mmoja kama
kianzio huku akiwaahidi kuwa mbegu za kutosha na viuatilifu kwa ajili ya maeneo
yao watapatiwa.
Akisistiza kaulimbiu
ya Singida mpya kwa pamba yenye tija amewataka Wanasiasa, watendaji wa serikali
na viongozi wa dini washirikiane na serikali kwa pamoja katika kutoa hamasa na
elimu ya kilimo cha pamba.
Dkt Nchimbi ametoa
onyo kwa wauza pembejeo na wasambaaji wasio waaminifu ambao husambaza dawa
zisizo halisi kuwa serikali itawabaini na kuwapa adhabu kali huku akiwataka
wakulima wasinunue dawa bila ushauri wa maafisa ugani.
“Kuna dawa nyingine
ukipuliza kwenye wadudu waharibifu wa pamba badala ya kufa wananenepeana, sasa
ole wako serikali ikukamate wewe unayemuuzia
mwananchi dawa feki hakika tuakushughulikia ipasavyo”, amesisitiza Dkt
Nchimbi.
Kwa upande wake Konyo
Mjika ambaye ni mkulima hodari wa pamba wilaya ya Iramba kutoka kijiji cha Msai
amesema msimu wa mwaka jana amelima ekari nane na kupata kilo elfu sita ambapo
ameweza kujenga nyumba nne za bati, kununua ng’ombe kadhaa na kuhudumia familia
yake.
Mjika ameongeza kuwa
ameweza kuvuna pamba nyingi kutokana na kusikiliza ushauri wa wataalamu wa
kupanda kwa kufuata mistari, kuweka mbolea na viuatilifu mapema.
Kutokana na mafanikio
hayo Mkulima Mjika amesema kwa msimu huu anatarajia kulima ekarini shirini
pamoja na kuwashauri wanakijiji wenzake walime pamba kwa wingi huku wakifuata
ushauri wa wataalamu ili waweze kuvuna kwa wingi.
Naye Zakaria Marko Mwakilishi
wa Kampuni ya Biosustain inayojihusiha na kilimo cha zao la pamba kwa mkataba amesema
kwa msimu huu kampuni hiyo itasambaza mbegu za pamba tani 300 mkoani Singida.
Marko ameongeza kuwa
uzalishaji wa pamba mkoani Singida umekuwa mdogo ukilinganisha na mahitaji ya
kiwanda chao ambapo mwaka jana zilipatitana kilo milioni 1 na mwaka huu zikaongezeka
hadi kilo milioni 1.5 kutokana na jitihada za wakuu wa wilaya, Mkuu wa Mkoa na
viongozi mbalimbai.
Ameongeza kuwa Kijiji
cha msai chenye wakulima wa pamba zaidi ya mia tano wameweza kuzalisha kilo laki
tano huku wilaya ya Iramba yote ikizalisha kilo laki nane na nusu kwa msimu wa
mwaka jana na mategemeo yakiwa makubwa zaidi kwa mwaka huu.
Marko amesema
kutokana na msukumo wa serikali na Viongozi wa Mkoa wa Singia ni matarajio yake
kiwanda cha Bio Sustain sasa kitazalisha kwa faida kutokana na kupata pamba ya
kutosha hapa Singida na sio kuifuata mikoa ya jirani kama ilivyokuwa hapo
awali.
No comments:
Post a Comment