Uchaguzi
wa Kamati ya Uongozi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) unafanyika
Jumapili, Oktoba 15 mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa
Taifa, jijini Dar es Salaam.
Wagombea
saba wamepitishwa kuwania uongozi wa TPLB baada ya Kamati ya sasa
kumaliza muda wote. Kamati mpya ya Uongozi itakayochaguliwa katika
uchaguzi huo unaosimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF utakaa madaraka
kwa kipindi cha miaka minne.
Waliopitishwa
kwenye kinyang’anyiro hicho baada ya orodha ya mwisho iliyotolewa
Oktoba 9, mwaka huu ni Clement Andrew Sanga kutoka Yanga na Hamad Yahya
Juma wa Mtibwa Sugar wanaowania uenyekiti wa TPLB.
Wengine
ni Shani Christoms Mligo wa Azam FC ambaye ni mgombea pekee wa nafasi
ya Makamu Mwenyekiti. Nafasi tatu za kuwakilisha klabu za Ligi Kuu
kwenye Kamati ya Uongozi zimevutia wagombea wawili; Hamisi Mshuda Madaki
(Kagera Sugar) na Ramadhani Marco Mahano (Lipuli).
Almasi
Jumapili Kasongo kutoka Ashanti United FC ni mgombea pekee
aliyejitokeza kuwania nafasi ya uwakilishi wa klabu za Ligi Daraja la
Kwanza. Klabu za Daraja la Kwanza zina nafasi mbili.
Klabu
za Ligi Daraja la Pili zina nafasi moja kwenye Kamati ya Uongozi ya
TPLB, na mgombea pekee aliyejitokeza kuwania nafasi hiyo Edgar William
Chibura kutoka Abajalo FC.
Jumla
ya wajumbe 44 watashiriki Mkutano huo wa uchaguzi wa Baraza Kuu la
TPLB. Wajumbe hao ni klabu 16 za Ligi Kuu, klabu 24 za Ligi Daraja la
Kwanza na wawakilishi wanne wa klabu za Ligi Daraja la Pili.
Nafasi
ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa kuwakilisha klabu za
Ligi Kuu zitapigiwa kura na klabu 16 pekee za Ligi Kuu.
No comments:
Post a Comment