MABUNGE ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
yametakiwa kutenga bajeti za michezo za kutosha ili kuongeza ufanisi wa
mashindano ya mabunge hayo yanayofanyika kila mwaka.
Kauli
hiyo ya kuzitaka nchi hizo imetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakiyembe wakati akifunga mashindano ya
nane ya michezo ya mabunge hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Alisema amepata taarifa kuhusu bajeti hivyo ni matumaini yake kuwa katika mashindano yajayo changamoto hiyo haitakuwepo.
Dk.Mwakiyembe
alisema ni jukumu la mabunge kutenga bajeti nzuri kwa ajili ya michezo
ili kuhakikisha kuwa yanashiriki bila hofu yoyote katika mashindano
mbalimbali.
Waziri alisema iwapo mabunge yatatenga bajeti inayotosheleza ni dhahiri kuwa ushindani utakuwepo wakati wa mashindano .
"Hamjasema
katika risala yenu kuhusu ufinyu wa bajeti lakini najya bajeti zenu ni
ndogo sana nadhani wakati umefika kwa kuwepo bajeti ya kutosha ya
michezo ili kuleta ufanisi," alisema.
Aidha,
alitoa rai kwa bunge kutumia wizara ya michezo ili kuweza kuweka
mazingira rafiki ya kuhakikisha ushiriki mkubwa wa wananchi katika
mashindano hayo kwa miaka ijayo.
Kwa
upande wake Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Dk Tulia Ackson alisema
mashindano hayo yanapaswa kutumika kudumisha mshikamano, umoja na
ushirikiano baina ya nchi zao na wananchi.
Dk.Ackson
alisema katika mashindano hayo ya nane ambayo yalishirikisha zaidi ya
wabunge na watumishi 800 kutoka nchi za Burundi, Uganda, Kenya, Bunge la
Afrika Mashariki (EALA) na Tanzania yalifana pamoja na changamoto
kidogo zilizotokea.
Alisema
mashindano hayo yanapaswa kuwa endelevu kwani yamekuwa na mchango
mkubwa katika kukuza umoja, ushirikiano na mshikamano kati ya nchi
wanachama.
"Mashindano
haya yalianza Desemba mosi na yamemalizika jana kwa mafanikio makubwa
sana naamini mashindano ya mwakani ambayo yatafanyika nchini Uganda
yataboreshwa zaidi," alisema.
Naibu
Spika alisema ni imani yake kuwa mashindano yajayo yatarekebisha kasoro
ambazo zimejitokeza hasa katika mchezo wa pete ambapo kulikuwa na
mgogoro kidogo.
Alisema
katika mashindano hayo michezo saba ilichezwa ambayo ni gofu, riadha,
pete, wavu, mpira wa miguu, kuvuta kamba na kutembea kwa kasi.
Dk.Ackson
alisema Bunge la Tanzania limefanikiwa kuibuka na vikombe vitatu
ambavyo ni vya kuvuta kamba, kutembea kwa kasi na mbio za kupokezana
vijiti wanawake.
"Uganda
wamepata vikombe katika mpira wa miguu, wavu wanawake na gofu huku Kenya
wakibuka videdea katika riadha wanaume na wanawake, wavu wanaume na
Burundi wakipata tuzo ya timu bora," alisema.
Mwenyekiti
wa Bunge Sports Club, William Ngeleja alishukuru Bunge la Tanzania
kufanikisha mashindano hayo kwa ufanisi na usalama wa kutosha na kwamba
sasa wanajiandaa na mashindano ya mwakani.
Ngeleja alisema ni matarajio yake kuwa changamoto zilizojitokeza zitafayiwa kazi kwenye mashindano mengine ya mwakani.
No comments:
Post a Comment