*Azindua Mpango wa Pili wa Huduma Jumuishi za Fedha
*Asema bado kuna fursa nyingi za kukuza uchumi
Dar es Salaam, Tanzania
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema uwepo wa uchumi imara na unaokua kwa kasi ni miongoni
mwa vigezo vinavyochangia ukuaji wa haraka wa sekta ya fedha nchini.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Alhamisi, Desemba 21, 2017) wakati akizindua Mpango wa
Pili wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Kifedha katika ukumbi wa Benki Kuu jijini
Dar es Salaam.
Akizindua
mpango huo unaotarajiwa kutekelezwa kuanzia mwaka 2018 hadi 2022, Waziri Mkuu
alisema uwepo wa miundombinu muhimu iliyojengwa na inayojengwa na Serikali; na
sekta binafsi katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya vijijini; na ongezeko la
watumiaji wa mitandao ya simu na huduma za mawasiliano ni kati ya fursa nzuri
iliyotajwa kwenye mpango huo.
“Kati ya
fursa nzuri iliyotajwa kwenye mpango huo ni uwepo wa uchumi imara na unaokua
kwa kasi. Tukijenga vizuri juu ya misingi hii tunaweza kupiga haraka hatua za
maendeleo katika sekta ya fedha na uchumi kwa ujumla wake,” alisema.
Alisema ameupitia
mpango huo na kubaini kuwa umeainisha changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi hii
katika harakati zake za kuongeza matumizi ya huduma za kifedha. Hata hivyo, Waziri
Mkuu alikiri kuwa mpango huo umeainisha fursa ambazo zinaweza kutumika ili
kukabiliana na changamoto hizo na hatimaye kuongeza matumizi ya huduma za
kifedha.
“Changamoto
zilizoainishwa ni pamoja na kuimarisha utawala wa matumizi ya fedha taslimu kwa
ajili ya malipo badala ya matumizi ya mifumo ya kielektroniki ya malipo;
kukosekana kwa utambulisho wa kipekee (unique identification) kwa Watanzania
walio wengi; uhalifu kwa njia za mtandao (cyber-crime); kukosekana kwa mifumo
madhubuti ya taarifa za kutosha za watumiaji wa huduma za fedha na dhamana zao;
na uelewa mdogo wa masuala ya kifedha,” alisema.
Aliwataka
wajumbe wa Baraza la Taifa la Huduma Jumuishi za kifedha waaandae mpango
mahsusi wa kutoa elimu vijijini kuhusu faida na umuhimu wa huduma jumuishi za
kifedha Tanzania, na akasisitiza kuwa kipaumbele kitolewe kwa makundi maalum ya
vijana na wanawake.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu alisema wataalam wa uchumi duniani wanaeleza kwamba jamii ambayo
imejijengea utamaduni wa kujiwekea akiba katika asasi za kifedha ina fursa
kubwa ya kupata maendeleo endelevu na ya haraka.
“Hii ni kwa
sababu uwekaji akiba ndiyo kiini na nguzo ya uwekezaji wa miradi ya maendeleo,
na bila uwekezaji wa miradi ya maendeleo, hakuna maendeleo. Nchi zote
zilizoendelea zimejijengea utamaduni huu wa wananchi wake wa kujiwekea akiba,”
alisisitiza.
Alitoa wito
kwa wajumbe hao kuhakikisha kuwa mpango huo unajikita zaidi katika kuimarisha
utamaduni wa Watanzania kujiwekea akiba kwa kila aina ya mapato ambayo mwananchi
anapata, iwe katika kilimo au biashara au ufugaji au uvuvi au shughuli nyingine
yeyote anayofanya ya maendeleo.
“Taarifa ya
Mpango wa Pili wa Huduma Jumuishi za Kifedha inaonyesha kuwa asilimia kubwa ya
Watanzania (watu wazima) wanamiliki simu za mkononi na wanatumia simu hizo
kufanya miamala ya kifedha. Kwa msingi huo, nashauri kuwepo kwa ushirikiano wa
karibu baina ya wadau wa taasisi za fedha na wadau wa TEHAMA ili kuimarisha
matumizi na mtandao wa kifedha vijijini ili iwe kichocheo cha uchumi,” alisema.
Mapema, Gavana wa Benki Kuu,
Prof. Benno Ndulu alisema matokeo ya tathmini iliyofanyika yanaonyesha kwamba
wananchi walio karibu na huduma za fedha wameongezeka kufikia asilimia 86 mwaka
2017 ya Watanzania (watu wazima) ikilinganishwa na asilimia 29 ya mwaka 2012.
Pia
alisema Watanzania wanaotumia huduma za fedha hasa kupitia asasi za kifedha na
mitandao ya simu wameongezeka kutoka asilimia 17 mwaka 2009 hadi asilimia 11
mwaka 2006, na hadi sasa (2017) takwimu zinaonyesha kwamba wananchi asilimia 65 wanatumia huduma za kifedha nchini.
“Kutokana
na mafanikio haya makubwa, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika na ya
sita duniani kwa kuweka mazingira bora ya utoaji na upatikanaji wa huduma za
kifedha kwa wananchi,” alisema.
Naye Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Mabenki Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB,
Dk, Charles Kimei alisema wenye mabenki wana haja ya kubadili mtazamo na kujikita
kwenye ngazi ya chini ambako kuna watumiaji wengi zaidi.
“Wenye
kampuni za simu wameonyesha kuwa inawezekana kufikisha huduma kwa watu wa chini
kupitia simu zao, nasi tukitumia vifaa hivyo tunaweza kuwafikia wananchi wengi
kwa kuwapa huduma zetu,” alisema.
Alitumia
fursa hiyo kuwaomba viongozi wa ngazi zote wakiwemo wa mikoa, wilaya na wabunge
walifanye suala la uwekaji akiba liwe ajenda kuu ya mikutano yao kwa kuwaelezea
wananchi umuhimu wa suala hilo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, DESEMBA 21, 2017
No comments:
Post a Comment