HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 25, 2018

TBA ITATHMINI UBORA WA JENGO LA KITUO CHA FORODHA CHA SIRARI-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Mbuge wa Butiama, Nimrod Mkono cheti cha shukurani kilichotolewa na wilaya ya Butiama ili kuthamini mchango wake mkubwa wa kujenga na kuchangia maendeleo ya elimu wilayani humo. Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye Chuo Kikuu cha Julius Kambarage Nyerere  kilichojengwa na mbunge huyo kikiwa na sekonda na kutokana na ubora wake kilibadilishwa kuwa Chuo Kikuu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 
 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mhandisi Elius Mwakalinga akafanye tathmini ya ubora ya jengo la kituo cha pamoja cha forodha cha Sirari kilichopo kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya.

Ametoa agizo hilo jana (Jumapili, Januari 21, 2018) katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya kikazi mkoani Mara, ambapo alimuagiza Mkurugenzi huyo afanye tathmini na kuishauri Serikali kama jengo linafaa kutumika.
Januari 17, 2018 Waziri Mkuu alikagua kituo hicho kilichopo wilayani Tarime kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya, ambapo alisema hajaridhishwa na ujenzi huo kwa kuwa upo chini ya kiwango.
Pia Waziri Mkuu alipokagua jengo hilo alijionea mwenyewe kuta za jengo hilo zikiwa na nyufa nyingi kuanzia ukutani hadi sakafuni na pia rangi za baadhi ya kuta zikiwa zimebanduka. Kituo hicho kilianza kujengwa mwaka 2011 na kukamilika mwaka 2014
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alizungumzia kuhusu miradi ya maji inayotekelezwa katika mkoa huo, ambapo alisema “Miradi mingi ya maji mkoani Mara ni ya hovyo na fedha nyingi zimetumika na wananchi hawajapata huduma hiyo.”
Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu aliwaelekeza viongozi wa mkoa huo ifikapo Januari 25, 2018 wamkabidhi taarifa ya mikakati waliyonayo ya kuondoa kero ya maji kwa wananchi.
Pia aliwaagiza Naibu Waziri, OR-TAMISEMI, Bw. Josephat Kandege na Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Profesa Kitila Mkumbo wabaki mkoani Mara ili wafuatilie miradi hiyo.
Alisema anahitaji hatua sahihi zichukuliwe kwa waliohusika katika kukwamisha miradi ya maji na watafutwe popote walipo akiwemo Mhandisi Emmanuel Masanja aliyekuwa Halmashauri ya wilaya ya Rorya na kuhamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Waziri Mkuu alisema mkoa huo una tatizo kubwa la maji hivyo ni  vema vyanzo vya maji vitunzwe ili visiharibiwe na shughuli za binadamu kama kilimo na ufugaji.
Aliongeza kuwa kutokana na usimamizi mbovu wa miradi ya maji, Serikali imevunja Bodi ya Maji ya MUWASA na viongozi waliohusika katika usimamizi huo pamoja na Wakandarasi husika wanahojiwa na vyombo vya dola.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATATU, JANUARI 22, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages