*Ataka takwimu
za kahawa ziwe tayari ifikapo Feb. 28
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Mji na Wilaya za
Mbinga wahakikishe kuwa wanaunda kanda za kilimo na kuwasambaza maafisa kilimo
wao badala ya kuwaacha wakae maofisini.
Ametoa agizo
hilo jana jioni (Ijumaa, Januari 5, 2018) wakati akizungumza na watumishi na
madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga pamoja na Halmashauri ya Mji wa
Mbinga, kwenye ukumbi wa Jumba la Maendeleo, mjini Mbinga.
“Mkurugenzi wa
TC na DC chuja maafisa kilimo ulionao na uhakikishe wanabakia watatu tu. Abaki
DALDO, mtu wa horticulture na
mthamini, wengine wote wasambaze kwenye kanda ili wasimamie wakulima wakiwa huko
huko. Hili litekelezwe na Mkuu wa Wilaya ulisimamie” alisema.
Aliwataka maafisa
kilimo wa zao la kahawa waende vijijini na kufanya sensa ili waweze kubaini
wana wakulima wangapi wanaozalisha kahawa. “Afisa kilimo wa wilaya lazima ujue kijiji
kina wakulima wangapi wa kahawa, na wana ekari ngapi? Na katika ekari hizo, ana
miche mingapi? Hii itaisaidia Serikali ijue inahitaji dawa za aina gani, mbolea
kiasi gani na miche mingapi kwa wakulima wake,” alisema.
“Ninataka hizi
takwimu ziwe zimekamilika ifikapo tarehe 28 Februari, mwaka huu,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amewataka maafisa ushirika wa wilaya hiyo wakasimamie uundwaji wa AMCOS mpya na
kuimarisha zile za zamani ambazo zinafanya kazi vizuri.
“Maafisa
ushirika ninataka nipate takwimu ya AMCOS very strong (ambazo ziko imara)
kwenye wilaya yako. Iifikapo tarehe 28 Febriari, takwimu hizi ziwe
zimekamilika. Kama kuna AMCOS nzuri ziimarisheni, itisha uchaguzi ili uanze na
uongozi mpya,” alisisitiza.
Aliwaeleza
watumishi na madiwani kwamba Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kurudisha
heshima ya zao hilo ambapo zamani iliweza kusomesha watoto kadhaa kwenda
sekondari kutokana na mfuko wa kahawa.
“Zamani zao la
kahawa lilikuwa likisomesha watoto wa wakulima, sasa hivi hakuna hata anayefaidika
na zao hili. Tunataka zao hili liwanufainishe wakulima, iinue uchumi wa
wanaMbinga, isomeshe watoto na iwezeshe wakulima kujenga majumba,” alisema.
Alisema kuanzia
msimu ujao wa Mei, Juni na Julai 2018, ununuzi wa kahawa utafanywa na vyama vya
msingi vinavyotambulika kwa maafisa ushirika.
Aliwaonya
watumishi wa Halmashauri hizo waache kutoa vibali vya ununuzi wa kahawa kwa
watu binafsi wanaomiliki kampuni za kununua kahawa. “Halmashauri ndiyo mnatoa
vibali vya kampuni kununua kahawa. Huu ni mwisho sasa. Hatuna mnunuzi binafsi
wala hatuna kampuni binafsi, hawa wote tukutane kwenye mnada,” alisema.
Alisema hataki
kuona watumishi wa Halmashauri wakionesha vibali vya kununua kahawa kama moja
ya chanzo cha mapato kwenye Halmashauri hizo. “Ni marufuku kuingiza vibali
kwenye mapato ya Halmashauri,” alisema.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI,
JANUARI 6, 2018.
No comments:
Post a Comment