HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 22, 2018

RAIS MAGUFULI SIKIA KILIO CHETU

NA MWANDISHI WETU

SISI ni wakazi wa Kata tano za Wilaya ya Kinondoni za Bunju, Makongo, Mbezi Juu, Mabwepande na Wazo. Sisi ni wananchi ambao tayari tulikwisha athiriwa na mradi wa bomba la maji la Ruvu Juu ambapo wakati wakipitisha mradi huo tulitakiwa kupisha mita tano kutoka katika mradi huo na tukatekeleza.


Hivi sasa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (Dawasa) imetoa notisi na kututaka tuondoke ndani ya mita 15 kutoka katika mradi wa bomba hilo jambo ambalo sio sheria, kwani sheria iliyopo inataka wanaopaswa kuondoka ni wale walio ndani ya mita 5.


Sisi wananchi tumeshangazwa na kusikitishwa na matamko yanayotolewa na Dawasa kwani ni wazi wanataka kutumia mabavu kutuondoa katika maeneo yetu.


Awali ulipoanza kutekelezwa mradi huo hatukupinga ndiyo maana wale waliokuwa ndani ya mita tano waliamua kuondoa na kuvunja nyumba zao kupisha mradi huo ambao umeshatekelezwa na kuanza kazi kwa kipindi cha miaka mitatu hadi sasa.


Kutokana na kushindwa kuelewana na Dawasa tumelazimika kukifikisha kilio chetu kwa Rais wetu mpendwa John Magufuli tunatambua kuwa busara na hekima aliyojaliwa na Muumba anaweza kutupatia ufumbuzi wa suala hili.


Hivi sasa hatuwezi kuishi kwa amani kutokana na muda wote kuwaza mahali pa kwenda iwapo Dawasa wataamua kutuvunjia nyumba zetu. Wengine ni wajane tuna familia zinazotuangalia hivyo kama tutabomolewa nyumba zetu hakika hakuna msaada mwingine utakaotuokoa.


Tunasema kweli kuwa msaada wetu uliobaki ni Rais Magufuli ambaye amekuwa mkombozi wa kutatua kero nyingi za watu wa chini kama sisi zinazozotukabili.


Rais Magufuli anavyowajali wanyonge ndiyo maana tumelazimika kufikisha kilio hicho kwake ili aweze kuwasaidia tusiweze kuondolewa katika maeneo haya ambayo ndiyo mkombozi wetu hatuna pengine pa kwenda.


Sisi ni wakazi wa Kata tano za wilaya ya Kinondoni, tunachoshangaza ni kuona Dawasa ikitunyima amani sisi tulioko katika Kata hizo wakati bomba hilo limepita katika maeneo mbalimbali ya wilaya hii.


Tunachojiuliza Mhe Rais Magufuli ni kwanini manyanyaso haya yanafanywa kwetu tu? Na sio maeneo mengine yanayopita bomba hilo?


Pia kinachotushangaza mradi huo umekwisha tekelezwa na unafanyakazi sasa hivyo kuna sababu zipi za Dawasa kutaka tuvunje nyumba zetu wakati mradi umeshafanyika?


Mhe Rais Magufuli maeneo haya kuna miradi mbalimbali zikiwemo shule ambazo zimekuwa zikipokea watoto wasio na uwezo na kusomeshwa bure, wapo yatima pia wanasomeshwa bure katika shule hizo hivyo iwapo Dawasa watabomoa miradi ya shule hizo ni uhakika kuwa watoto waliopo katika shule hizo watakosa masomo.


Rais Magufuli sisi wananchi tunachotambua kuwa Mamlaka hiyo inapaswa kubomoa nyumba zilizo katika mita tano kushoto na kulia kama sheria ya mwaka 2001 ilivyoagiza na sio vingine.


Tunakuomba Rais Magufuli uingilie kati suala hilo ili haki iweze kutendeka kwetu sisi wananchi wa chini kwani kama Dawasa inahitaji kupata ardhi zaidi kwa ajili ya mradi huo basi wanachopaswa kufanya ni kufuata sheria ikiwa ni pamoja na kutulipa fidia ili waweze kuchukua maeneo hayo lakini sio kutumia nguvu na vitisho kama inavyofanyika sasa.


Tumaini letu ni kwako Rais Magufuli utakayeweza kutuokoa na janga hili ambalo linasababisha tuishi kwa hofu huku tukishindwa kufanya shughuli zetu za kila siku kwa kuhofu tukiondoka Dawasa wanawez kuingia na kubomoa makazi yetu.


Pia tunatambua kuwa wapo baadhi ya watendaji wamekuwa waking’ang’ania jambo hilo kwa lengo la kutaka kutukosanisha na serikali yako nasi hatupo tayari kuona jambo hilo likifanikiwa ndiyo maana tumelazimika kukibilia kwako.


Tunakombea Mungu akupe nguvu na afya tele ili uzidi kututetea sisi wananchi wanyonge wa chini ambao tegemeo letu ni kwako Rais Magufuli.


Tunatanguliza shukrani zetu


Ni sisi wananchi wa Kata tano

za jijini Dar Es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Pages