WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inasimamia kwa karibu
miundombinu ya elimu nchini, malezi na nidhamu ili kuhakikisha kunakuwa na usawa
katika ngazi zote.
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Alhamisi, Mei 17, 2018) Bungeni mjini
Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati
akijibu swali la Mbunge wa Muheza, Balozi Adadi Rajab aliyetaka kujua Serikali
imechukua hatua gani kudhibiti ubora wa elimu inayotolewa kwenye shule binafsi
ikiwemo nidhamu na malezi.
Waziri Mkuu amesema licha ya kuwa Serikali imetoa fursa ya uwekezaji
kwenye sekta ya elimu na kuruhusu watu binafsi waweze kuendesha shule au vyuo,
haina maana kuwa kila mtu ana uwezo wa kuendesha shule kadri apendavyo.
Amesema Serikali inasimamia kwa karibu miundombinu ili kuona kama inakidhi
mahitaji ya taasisi iliyokusudiwa; inachunguza kama imesajiliwa; inafanya
ukaguzi wa mazingira ya mahali taasisi ilipo, iloi kubaini kama ina eneo la kutosha
na mazingira hayo yanaruhusu kutolea taaluma.
“Jambo jingine ambalo tunasisitiza ni kwamba; kama mwekezaji huyo
amekubali kuwekeza kwenye elimu ya msingi, sekondari au chuo, atalazimika
kufuata mitaala ya kiserikali; ili afundishe mtaala ambao pia unafundishwa
kwenye shule za Serikali na watoto wote wapate elimu inayofanana,” amesema Waziri
Mkuu.
Amesema Serikali inafanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kubaini kama elimu
inayotolewa na taasisi husika ina kiwango sawa na taasisi nyingine kwa sababu
mwishoni kuna mitihani inayotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa ili kupima kama
elimu waliyoipata inafuata mtaala mmoja na kama ina viwango vinavyotakiwa.
Akitoa ufafanuzi kuhusu suala la malezi na nidhamu, Waziri Mkuu amesema suala
hilo linawekewa msisitizo kwa sababu ndilo linajenga vijana ambao watakuwa
viongozi wa baadaye. “Lengo letu ni kuona elimu inaboreshwa, inawiana kote
nchini na wawekezaji wanakaguliwa ili kutotofautisha viwango na ubora wa elimu
inayotolewa nchini,” amesema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
ALHAMISI, MEI 17,
2018.
No comments:
Post a Comment