SERIKALI imewaasa viongozi wa dini waeuepuke
migogoro ya mara kwa mara katika Makanisa yao na badala yake waendelee kuwajenga
waumini wao wakue kiroho na kujenga dhana ya umoja na upendo katika Taifa.
Pia imesema inawashukuru viongozi wa dini na
madhehebu yote ya dini kwa kuendelea kuiombea nchi amani, mshikamano na utulivu,
jambo ambalo linaongeza chachu kubwa kufikia mafanikio ya maendeleo ya kijamii,
kisiasa na kiuchumi.
Hayo yamesemwa leo (Jumapili, Mei 20, 2018) na
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika ibada ya kutawazwa Askofu Dkt. Maimbo
Mndolwa wa Dayosisi ya Tanga kuwa Askofu Mkuu wa saba wa Kanisa la Anglikana
Tanzania. Ibada hiyo imefanyika katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu Dayosisi ya
Central Tanganyika Jijini Dodoma.
“Nawaombeni
wote kwa ujumla wetu, tuendelee kutumia Makanisa yetu kuombea Taifa hili ili tuendelee
kuishi kwa amani, upendo na mshikamano”. Watu wa Mungu ni watu wa Upendo, watu
wa Mungu ni watu wa amani, watu wa Mungu ni watu wa kiroho”.
Waziri Mkuu
ameongeza kuwa “haitarajiwi kuona watu wa Mungu wakiwa katika mstari wa mbele kuchochea
migogoro, kuvunja amani ya Kanisa na kuongoza makundi yanayopingana katika kazi
ya Bwana”.
Amesema
jukumu la makanisa ni kuwajenga waumini kukua kiroho, na kazi ya kuwaongoza
watu wamjue Mwenyezi Mungu, ambapo amewaomba imani yao iwe moja na matendo yao
yafanane na yale ya Kristo Yesu wanayemuamini.
Waziri Mkuu
amesema kuwa nchi haiwezi kupata mafanikio ya kiuchumi na kijamii bila kuilinda
amani iliyopo, hivyo amewaomba warejee kumbusho la maandiko Matakatifu katika Waebrania
12:14 “Tatufeni kwa bidii kuwa na Amani
na watu wote”.
Pia Waziri
Mkuu ametoa wito kwa viongozi hao na wananchi kwa ujumla waendelee kuwaombea viongozi
wa Tanzania hususani Rais Dkt. John Magufuli, kuendelea kuwa na afya njema,
busara, upendo, hekima katika kuiongoza nchi yetu.
Waziri Mkuu
ambaye amemuwakilisha Rais Dkt. Magufuli katika ibada hiyo amesema Serikali
inatambua ushirikiano uliopo kati ya madhehebu mbalimbali ya dini nchini kwa
ujumla wake na kwamba ushirikiano huo ni wa kihistoria.
Amesema mara
zote madhehebu ya dini yamekuwa yakisaidiana na Serikali katika kutoa huduma za
elimu, afya, maji na makundi maalum kama vile yatima, wazee, walemavu, wajane
na huduma hizo zimekuwa zikitolewa kwa Watanzania wote bila ubaguzi wa aina
yoyote. “Mambo haya hayawezi kupatikana nchini bila ya kuwa na amani”.
Kwa upande
wake Askofu Dkt. Mndolwa baada ya kutawazwa aliahidi kulitumikia kanisa la
Anglikana katika kweli, haki na upendo.
“Naahidi kwa
makini kwamba nitaistahi na kudumisha na kuilinda Imani, haki na uhuru wa Kanisa
la Anglikana Tanzania na kulitumikia katika kweli, haki na upendo, nisijifanye
kuwa bwana juu ya urithi wa Mwenyezi Mungu, bali katika mambo yote nioneshe
kielelezo kwa kundi la Kristo. Mungu nisaidie,”.
Askofu Dkt.
Mndolwa anashika wadhifa huo baada ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la
Anglikana Tanzania Askofu Jacob Chimeledya kumaliza muda wake. Askofu
Chimeledya alitawazwa mwaka 2013.
Maaskofu
wengine waliowahi kuongoza kanisa hilo tangu kuasisiwa kwake nchini ni John
Thomas Mhina Sepetu (1970-1978), Askofu Musa Kalemo Kahurananga (1979-1983),
Askofu John Auckland Ramadhani (1984-1997), Askofu Donald Leo Mtetemela
(1998-2008), Askofu Valentino Leonard Mokiwa (2009-2013).
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMAPILI, Mei 20, 2018.
No comments:
Post a Comment