WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa yote nchini washirikiane
na wadau wa mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kuanzisha kampeni ya
kuhamasisha wananchi hususani wanaume kupima VVU na kuanza kutumia dawa
mapema.
Kadhalika,
amewaagiza Wakuu hao wa Mikoa na Wilaya kwa kusaidiana na Wakurugenzi
wa Halmashauri zote nchini wasimamie kwa uzito unaostahili kampeni hiyo
itakayoendeshwa kwa muda wa miezi sita mfululizo.
Waziri
Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumanne, Juni 19, 2018) wakati akizindua
kampeni ya Kitaifa ya kuhamasisha wananchi hususani wanaume kupima VVU
na kuanza kutumia dawa mapema, iliyofanyika katika Uwanja wa Jamuhuri,
jijini Dodoma.
“Kwa vile tunazindua kampeni ya kupima na kuanza ARV mara moja (Test and Treat)
natoa rai kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI, mhakikishe vitendanishi na dawa
za ARV zipo za kutosheleza katika kila kituo kinachotoa huduma katika
kila Mkoa na Wilaya,” amesema.
Waziri
Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahamasisha watu wote watakaogundulika na
maambukizo ya VVU waelewe kuwa utaratibu wa sasa ni kuanza dawa mara
moja pasipo kujali kiwango cha kinga mwilini, yaani CD4.
Amesema
huo ni utaratibu ambao nchi imeuridhia kwa kuwa una manufaa kwa
mtumiaji wa dawa na jamii kwa ujumla. “Mtu yeyote asisite kuanza dawa
mara tu anapogundulika kuwa na maambukizo ya VVU bila hata kusubiri CD4
kushuka sana,”.
Katia hatua nyingine,
Waziri Mkuu ametaja baadhi ya njia zitakazosaidia kuwafikia wanaume kwa
ajili ya kupima VVU na kuanza dawa mara wanapogundulika kuwa na
maambukizi kuwa ni pamoja na kupanua wigo wa kuwatumia wanaogundulika na maambukizi ya VVU kuwaleta wenza wao sehemu za kupata huduma.
“Kuimarisha
fursa ya wahudumu wa afya kwa magonjwa mengine, kuwashawishi watumiaji
wa huduma hizo kupimwa VVU, hususan wanaume na kupanua huduma za upimaji
na ushauri nasaha hasa katika Mikoa na Wilaya zenye maambukizo makubwa
ya VVU lakini ikiwa na watu wachache wanaojua hali zao za maambukizo,”
amesema.
Pia
kuainisha na kutumia maeneo ya shughuli za kiuchumi, kijamii, kidini,
kimila na starehe yanayowaleta wanaume pamoja ili kuwahamasisha wanaume
(wazee na vijana) kuziendea huduma za upimaji wa VVU na magonjwa mengine
sugu.
Waziri
Mkuu amesema anaamini utaratibu huo utaleta matokeo chanya hasa kwa
kuwatumia wanaume ambao ni viongozi na wanaoheshimika katika maeneo
husika pamoja na kuziunganisha huduma za upimaji wa VVU katika upimaji
na huduma za magonjwa mengine kama magonjwa yasiyo ya kuambukizwa ili
kuimarisha upatikanaji wa huduma katika sehemu mmoja.
Waziri
Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wadau wote wa mapambano ya VVU
na UKIMWI kwamba Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais chini
ya uongozi Dkt. John Magufuli, itaendelea kufanyanao kazi kwa karibu ili
kwa pamoja wafikie lengo ya kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
Uzinduzi
huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,
Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama, Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bibi Ummy Mwalimu na
Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Bw. Suleiman Jafo.
Wengine
ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana,
Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Bw. Anthony Mavunde, Naibu Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye
Ulemavu, Bibi Stella Ikupa, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
Kuhusu Masuala ya UKIMWI, Bw. Oscar Mukasa.
Makatibu
Wakuu wa Wizara, Viongozi na Watendaji Wakuu wa Serikali, Mkurugenzi
Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Dkt. Leonard Maboko,
Wadau wa Maendeleo, Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya
UKIMWI (NACOPHA), Bw. Justin Mwinuka, Viongozi wa Dini na Asasi za
Kiraia, Wakuu wa Mikoa na Wilaya.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMANNE, Juni 19, 2018.
No comments:
Post a Comment