Kamati ya watu wenye ulemavu Mkoa wa Rukwa imeaswa
kuhakikisha inawatambua watu wenye ulemavu na kubaini mahitaji yao pamoja na
kuona namna ya kutatua changamoto zao ili kuweza kuwasaidia katika kufikia
malengo yao katika sekta mbalimbali za kimaendeleo.
“Katika Mkoa wa Rukwa tunachamoto kubwa juu ya namna ya
kuwahudumia watu wenye ulemavu, kwani mara nyingi watu hawa wamekuwa wakileta
malalamiko yao katika ofisi hii, hivyo uwepo wa kamati hii utapunguza sana
changamoto wanazokabiliana nazo ndugu zetu hawa.”Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa
wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alipokuwa akizindua kamati ya watu wenye ulemavu
ngazi ya Mkoa.
Ameongeza kuwa ni matumaini ya serikali kuwa kamati hiyo itazisimamia
kamati zote zilizopo chini yake kuanzia ngazi ya halmashauri, mitaa na vijiji
ili kujua idadi ya watu wenye ulemavu kuanzia ngazi ya kitongoji hadi kufikia
ngazi ya halmashauri na kupeleka taarifa ya utekelezaji wa majukumu yao kwa
Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Kwa upande wake akisoma taarifa ya kamati katibu wa
kamati ya watu wenye ulemavu mkoa Godfrey Mapunda amezitaja changamoto mbalimbali
zinazowakabili watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kutokuwa na taarifa sahihi
juu ya haki zao, kutokuwepo kwa miundombinu isiyozingatia hali za watu wenye
ulemavu zinazowapelekea kushindwa kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za
kijamii pamoja na Imani potofu kwa jamii inayowapelekea kushindwa kupata elimu
na mahitaji muhimu.
Na kueleza majukumu ya kamati hiyo ikiwa ni pamoja na “Jukumu
la kwanza itakuwa ni kutambua haki na uwezo wa watu walio na ulemavu katika
mkoa lakini pia kuwasaidia watu wenye ulemavu na familia zao na kupanga mipango
yenye ufanisi ili kupunguza umasikini kupitia shughuli za kujiingia kipato,
kuratibu shughuli zote za watu wenye ulemavu katika mkoa, kulinda na kukuza ustawi
wa watu wenye ulemavu katika Mkoa,” Alisema.
Hadi kamati hiyo inazinduliwa na Mkuu wa Mkoa asilimia 42
ya kamati za watu wenye ulemavu kuanzia ngazi ya Kijiji hadi halmashauri
zilikuwa zimeshaundwa na walemavu 774 wamebanika huku maazimio ya kamati hiyo
ikiwa ni kuhakikisha kamati zinaundwa kwa asilimia 100 na walemavu wote
kutambulika na kuwa na takwimu sahihi ili kuweza kuwafikishia huduma stahiki.
Hii ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Mh.
Kassim Majaliwa alilolitoa alipohudhuria hafla ya chakula cha mchana
kwa watu wenye ulemavu iliyoandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya
IPP, Bw. Reginald Mengi kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee mapema mwezi wa pili
mwaka 2018.
Maelezo ya Picha
Mwenyekiti wa Kamati ya Watu wenye Ulemavu
Mkoa wa Rukwa Lt.Col. John Antonyo Mzurikwao akiendesha kikao chake cha
kwanza cha kamati hiyo tangu kuteuliwa kwake na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa
mwezi wa tano mwaka 2018.
IMETOLEWA NA
OFISI YA MKUU WA MKOA WA RUKWA
No comments:
Post a Comment