Waziri wa Fedha na
Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor. Mpango (Mb) (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa
Benki ya NMB Bi. Ineke Bussemaker, wakipeana mkono wakati wa makabidhiano ya hundi
kifani yenye thamani ya shilingi bilioni 10.1, ambayo ni gawio lililotolewa na
Benki ya NMB kwa Serikali, Jijini Dodoma. (Picha
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango).
Na
Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Benki
ya NMB imetoa gawio la Sh. bilioni 10.1 kwa Serikali ambayo inamiliki asilimia
32 ya hisa za Benki hiyo baada ya kupata
faida ya Sh. bilioni 94.8 baada ya kodi kwa mwaka 2017/2018.
Tukio
hilo la kukabidhi hundi kifani ya gawio hilo limefanyika Makao Makuu ya Wizara
ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma, kati ya Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Philip Mpango, kwa niaba ya Serikali, na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki
hiyo Ineke Bussemaker.
Dkt.
Mpango amezipongeza juhudi za watendaji wa Benki hiyo waliofanikisha kupatikana
kwa faida iliyowezesha Serikali kupata gawio licha ya changamoto zilizoikumba
Sekta ya Benki likiwemo suala la mikopo chechefu.
“Mikopo
chechefu imekua tatizo kwa Benki nyingi nchini hivyo ninatoa rai kwa Benki ya
NMB kuhakikisha inafuata taratibu za kukopesha na kuendelea kusimamia vizuri
wakopaji ili kuondoa tatizo la mikopo chechefu” alieleza Dkt. Mpango.
Aidha
ameipongeza Benki hiyo kwa kutoa huduma katika Sekta ya kilimo na kuitaka
ipanue wigo zaidi na kuziwezesha sekta za uvuvi na ufugaji kutokana na umuhimu
wake katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Alisema
kuwa anatarajia Benki hiyo itatoa gawio zaidi mwaka ujao wa fedha na amemwagiza
Msajili wa Hazina, kuzihakiki taasisi zote ambazo Serikali imewekeza hisa zake
ili zitoe gawio lasivyo ametishia Serikali kuondoa hisa zake kwakuwa uwekezaji
huo hautakuwa na tija.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Ineke Bussemaker alieleza kuwa
licha ya Benki yake kutoa gawio hilo la shilingi bilioni 10.1 kwa Serikali, pia
inalipa kodi za Serikali vizuri ambapo katika kipindi cha mwaka 2017/18 imetoa
kodi ya shilingi bilioni 127.
Aliongeza
kuwa tangu mwaka 2014 hadi 2017 benki hiyo imetoa kodi zinazofikia zaidi ya
shilingi bilioni 460 na kwamba itaendelea kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma
za kibenki ili iweze kupata faida na kulipa gawio kubwa zaidi kwa wana hisa
wake ikiwemo Serikali inayomiliki silimia 31.8 ya hisa 500.
Aidha,
amesema kuwa Benki yake imeendelea kufanya kazi kwa karibu na Sekta ya Kilimo
kwa kutoa huduma za kifedha kwa wakulima wakiwemo wakulima wa Tumbaku na
Korosho katika mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara, ambapo imefungua zaidi ya
akaunti 300,000 na kuweza kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 250 mwezi Novemba
mwaka jana.
Bi.
Bussemaker alisema kuwa Benki yake inajitahidi kuhakikisha kunakua na huduma
jumuishi za kifedha kwa wananchi kote nchini kwa kuweka Mawakala na kuongeza Matawi
ya Benki hiyo na pia kuhamasisha wananchi wafungue Akaunti ya Benki hiyo.
Alisema
kuwa ili kufanikisha utoaji wa huduma hiyo ya kifedha kwa watanzania, Benki
hiyo imejipanga kutumia teknolojia ya kisasa ya masuala ya fedha ambayo
itarahisisha kuwafikia watu wengi ikiwemo
huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi.
Katika
Mwaka wa Fedha 2016/2017, Benki hiyo ilitoa gawio la shilingi bilioni 16.5 kwa
Serikali, huku kukiwa na pungufu ya shilingi bilioni 6 mwaka huu hatua
iliyomlazimu Dkt. Mpango kuiagiza Benki hiyi ihakikishe inaboresha huduma zake
ili Serikali ipate gawio kubwa zaidi kwa ajili ya kutumia fedha hizo kuwaletea
wananchi maendeleo katika sekta za maji, afya, elimu, na miundombinu mingine
muhimu.
No comments:
Post a Comment