WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amefanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika Mheshimiwa
Stephen Masele na kumuahidi kwamba Serikali itampa ushirikiano ili aweze kutimiza
majukumu yake.
Ametoa ahadi
hiyo leo (Jumanne, Juni 5, 2018) wakati akizungumza na Mheshimiwa Masele ofisini
kwake Bungeni, Dodoma. Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza kwa
kuchaguliwa kushika wadhifa huo.
Amesema ushindi
wake katika nafasi hiyo umelipa heshima kubwa Bunge na Serikali na kwamba wana matarajio
makubwa kwa sababu uwepo wake, utaliongezea Taifa ushirikiano na nchi nyingine za
Afrika.
"Matarajio
kwa Bunge ni makubwa kwani kuna mambo ambayo tunataka ushirikiano na nchi nyingine
za Afrika, hivyo uwepo wako ni muhimu katika kufanikisha utekelezaji wake."
Vilevile,
Waziri Mkuu amewapongeza wabunge wengine wawili, Waheshimiwa David Silinde na
Asha Abdullah Juma kwa ushirikiano wao uliochangia ushindi wa Mheshimiwa
Masele.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Masele ambaye ni
Mbunge wa Shinyanga Mjini, ameishukuru Serikali kwa ushirikiano iliyompa na
hatimaye kuibuka na ushindi huo.
Amesema ushindani
ulikuwa mkali kutokana na uwepo wa mataifa mengi yaliyokuwa yakiwania nafasi
hiyo. Aliahidi kutetea maslahi ya Taifa kwa muda wote atakaotumikia nafasi
hiyo. “Nakuhakikishia Waziri Mkuu kwamba nitayalinda na kuyatetea maslahi ya
Tanzania kwa muda wote ambao nitakuwa katika wadhifa huu,” alisema Mhe. Masele.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU,
S.
L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMANNE, JUNI 5,
2018.
No comments:
Post a Comment