HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 07, 2018

WAZIRI MKUU AZIONYA ASASI ZISIZO ZA KISERIKALI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka asasi zisizokuwa za Serikali (NGOs) zitekeleze majukumu yake kama ambavyo zimesajiliwa na ziache kufanya shughuli zilizo nje ya makubaliano.

Amesema Serikali itaendelea kuzichukulia hatua NGOs zote zinazokiuka taratibu kwa kufanya majukumu mengine kinyume na malengo yake.

Ametoa onyo hilo leo (Alhamisi, Juni 7, 2018) Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Longido, Dkt. Stephen Lemomo Kiruswa kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

“Serikali itaendelea kuzifuatilia NGOs zote zinazokiuka taratibu na kufanya majukumu mengine yanayozua mitafaruku kwenye jamii na Serikali,” amesema.

Dkt. Kiruswa alitaka kufahamu ni lini Serikali itazifutia usajili NGOs zote ambazo kwa muda mrefu zimeacha kutekeleza majukumu yake na badala yake zinafanya shughuli za uchochezi.

Waziri Mkuu amesema Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ina utaratibu wa kufuatilia taasisi hizo kubaini endapo zinafanya kazi kama zilivyojieleza kwenye usajili wake.

Amesema mara inapobainika kwamba kuna NGOs ambazo zimeacha majukumu yake na zinafanya shughuli zingine nje ya mikataba yao, hatua stahiki huchukuliwa, hivyo alizitaka zijikite katika utoaji wa huduma bora kwa jamii.

“Kwa hiyo nitoe wito kwa NGO’s zote ambazo Serikali imeridhia na tumezisajili ili ziweze kufanya kazi ya kutoa huduma za jamii, zijikite kutoa huduma za jamii kama ambavyo tumekubaliana, ili tuweze kufikia malengo ya pamoja kati ya Serikali na taasisi zisizo za kiserikali katika kutoa huduma kwa Watanzania wote,” amesema.

Akitoa mfano wa hatua ambazo zimeshachukuliwa na Serikali kwa asasi zinazokiuka makubaliano, Waziei Mkuu amesema aliwahi kuzuru wilaya ya Loliondo na kukuta kuna utitiri wa NGOs ambazo zilikuwa zinaenda kinyume na malengo yaliyokusudiwa.

“Niliwahi kutembelea wilaya jirani na yako pale Loliondo; nilikuta kuna NGOs 39 katika wilaya moja tu. Na kulikuwa na migogoro kadhaa ambayo baadhi ya NGO’s, kama ambavyo umesema, zimekuwa zikiacha majukumu yake na kufanya majukumu mengine ambayo ni nje ya utaratibu tuliokubaliana. Kauli niliyotoa, ilikuwa kwanza kuwatahadharisha, lakini pili tulipeleka wakaguzi kujiridhisha kama ni kweli jambo hilo linafanyika; na tatu tulichukua hatua kwa NGO’s ambazo zilibainika kujishughulisha na mambo mengine nje ya kazi zao,” amesema.

Amesema anatambua mchango unaotolewa na NGOs katika kuisadia Serikali kutoa huduma za jamii kwenye maeneo mbalimbali hasa yale ambayo Serikali haitamudu kufanya kila kitu kwa asilimia 100. “Serikali imezipa fursa taasisi hizi zisizokuwa za kiserikali, zenye fursa na utaalamu wa kutoa huduma kwa jamii, na sisi tumetoa ruhusa kisheria kabisa kwa kusajili taasisi hizo ili ziweze kufanya kazi hizo,” amesema.

“Sasa kwa kuwa taasisi hizi zimesajiliwa, na taasisi hizi zina malengo, na malengo yale ndiyo yaliyofanya tuwape kibali ili ziweze kusajili, naamini kila NGO’s inajua wajibu wake. Zitimize wajibu wake ili tuweze kufikia malengo ya pamoja kati ya Serikali na taasisi zisizo za kiserikali,” amesisitiza.
 
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
ALHAMISI, JUNI 7, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages