HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 29, 2018

MA-DED MKOANI TABORA WATAKIWA KUPANGISHA VIBANDA KWA BEI SOKO NA SIO CHINI YA HAPO

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nzega Mjini, Philemon Magesa, akichangia mada jana wakati wa kikao kazi cha Wakurugenzi Watendaji na baadhi ya mofisa  wa halmashauri zote nane cha kujadiliana Mpango Mkakati wa kuboresha ukusanyaji mapato kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa Mkoani Tabora kwa mwaka wa fedha wa 2018/19 ili ziweze kufikia lengo lilowekwa. (Picha na Tiganya Vincent).

NA TIGANYA VINCENT, TABORA

WAKURUGENZI Watendaji katika  Halmashauri zote za Mkoani Tabora wameagizwa kuangalia uwezekano wa kupangisha vibanda na majengo ya kuweka maduka kulingana na bei ya soko na sio chini ya hapo ili kuziongeze mapato yake ya ndani.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu wakati wa kikao kazi cha siku moja na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Tabora na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya na ile ya Mji wa Nzega cha kujadiliana jinsi ya kuboresha ukusanyaji mapato.

Alisema kila Mkurugenzi Mtendaji katika eneo lake wakae na Wataalamu wao wanaohusika na ukusanyaji wa mapato ili kuona jinsi wanavyoweza kukusanya mapato yanayotokana na upangishaji wa vibanda wanavyomiliki kulinga na bei halisi ya soko  na eneo lao.

Makungu alisema kuendelea kupokea pesa chini ya hali halisi ya soko haiwezi kuzisaidia Halmashauri husika kujiandaa katika kuelekea kuwa na mapato ya kutosha ambayo yataziwesha kujitegemea katika uendeshaji wa shughuli zake kwa asilimia 100.

Aidha Katibu Tawala huyo wa Mkoa aliwataka kuhakikisha wanasimamia haki katika ukusanyaji wa mapato na kuongeza kuwa kama kutaweko na vikwazo ni vema waweeleze wakuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa ili awasaidie.

“Kama kikwazo ni Diwani au mwanasiasa toeni taarifa ili tumuripoti kwa mamlaka zake za nidhamu ili achukuliwe hatua kulingana na taratibu za chama chake kwa kuzuia ukusanyaji wa mapato” alisema.

Naye Katibu Tawala Msaidizi  Nathalis Linuma alizitaka Halmashauri zote Mkoani humo kujiimarisha katika ukusanyaji wa mapato yake ya ndani ili ifikapo mwaka 2025 ziweze kujitegemea kwa asilimia 100 na hivyo kuwa na fedha zitakazo waweesha katika uendeshaji wa shughuli zake bila kutegemea Serikali kuu.

Alisema hatua hiyo itafikiwa ikiwa watasimamia kwa weledi ,uaminifu na uzalendo ukusanyaji wa mapato katika vyanzo vilivyopo na kubuni vyanzo vipya ambavyo vilikuwa hatozwi ushuru wa huduma lakini vilipaswa kutozwa.

Kwa upande wa Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora Richard Lugomela alisema baadhi ya Halmashauri Mkoani humo zimeshindwa kufanya vizuri katika makusanyo kwa sababu ya kushindwa kukusanya ushuru wa huduma katika baadhi ya maeneo na hivyo kuzikosesha Halmashauri zao mapato ya ndani.

Alitaja vyanzo ambavyo baadhi ya Halmashauri Mkoani humo zimeshindwa kukusanya licha ya wao kufanyabiashar ni pamoja na Shule za Binafsi na zile za madhehebu ya dini, nyumba za kulala wageni na hoteli, Kampuni za umma na Taasisi za Umma ambazo zinafanyabiashara na maeneo ya viwanja ambayo yamekuwa yakitumiwa na wamiliki kibiashara.

No comments:

Post a Comment

Pages