MKE wa Waziri Mkuu, Mama
Mary
Majaliwa amewaongoza wake wa viongozi kuchangia sh. milioni nne kwa ajili ya
watoto wawili wanaohitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo.
“Kwa umoja wetu, na kwa
kuguswa na uhitaji wa watoto wenye matatizo ya moyo, tuliamua tuchange fedha na
zimefikia shilingi milioni nne ili tuweze kusaidia kuchangia gharama za
matibabu kwa ajili ya watoto wawili,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa,
Julai 27, 2018) wakati akizungumza na baadhi ya wazazi na watumishi wa Taasisi
ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili mara baada ya kuwatembelea
watoto wengine waliofanyiwa upasuaji wiki hii.
Mama Majaliwa ambaye
aliongozana na wake wengine wa viongozi wakiongozwa na Mwenyekiti wa New Millenium Group, Mama Mbonimpaye Mpango,
alikabidhi hundi kwa wazazi wa watoto wawili ambao ni Angela Francis (2) na Sabina
Mnyango (4).
Watoto hao ni miongoni mwa
watoto tisa wenye umri wa miezi mitatu hadi miaka 17 ambao walipangiwa kufanyiwa
upasuaji wa kufungua kifua na madaktari bingwa wa JKCI kwa kushirikiana na
wenzao kutoka Shirika la Chain of Hope
la Uingereza. Matibabu hayo yalianza Julai 23, mwaka huu na yanatarajiwa
kukamilishwa leo.
Mama Majaliwa aliwashukuru madaktari
na wauguzi wa JKCI kwa uamuzi wao wa kuwafanyia matibabu watoto hao hapa nchini
kwani kwa kufanya hivyo wameokoa fedha za Serikali ambazo zingetumika kumtibu
kila mtoto kama wangeamua kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu.
Pia alimshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Serikali ya
awamu ya tano kwa jinsi wanavyoendelea kuimarisha utoaji wa huduma kwenye sekta
ya afya hasa kwa mama na mtoto.
Amesema gharama ya matibabu ya
mgonjwa mmoja anapopelekwa nje ya nchi kwa siku 14, inakaribia wastani wa sh.
milioni 30. “Kwa kuamua kufanya upasuaji huu hapa nchini, mmeongeza faraja kwa
watoto wetu; mmewawezesha ndugu na wanafamilia kuwa karibu zaidi na mgonjwa wao
tofauti na hali ambavyo ingekuwa kama upasuaji huo ungefanyika nje ya nchi,”
amesema.
Mama
Majaliwa amesema inakuwa vigumu kwa mzazi kutambua mtoto yupi amezaliwa na
tatizo la kwenye moyo pindi tu anapozaliwa. “Takwimu zilizopo zinaonyesha
kwamba katika kila watoto 100 wanaozaliwa, mtoto mmoja huwa anazaliwa akiwa na
tatizo kwenye moyo wake,” amesema.
Mapema, akitoa taarifa fupi kuhusu
taasisi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Prof. Mohamed Janabi alisema wagonjwa
wote waliofanyiwa upasuaji wanaendelea vizuri na watoto sita wameruhusiwa
kutoka katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) na kupelekwa wodini kuendelea
na matibabu.
Hii ni mara ya tatu kwa
matibabu ya moyo kwa watoto kufanyika tangu Januari mwaka huu. Mara ya kwanza madaktari
wa JKCI walishirikiana na wenzao kutoka Uingereza; mara ya pili ulifanyika
upasuaji wa moyo bila kufungua kifua ambapo wa Save a Child’s Heart (SACH) kutoka Israel na Berlin Heart Centre ya Ujerumani walishiriki na mara ya tatu
walishirikiana na taasisi ya Open Heart International
(OHI) ya Australia.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wazazi
wa watoto hao, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto, Dk. Nice Majani
aliwashukuru akinamama hao kwa uamuzi wao wa kuwasaidia watoto wasio na uwezo wa kuchangia matibabu
hayo.
“Tunawashukuru sana kwa
msaada wenu kwa sababu kuna wazazi wengine wanashindwa kupata kama hizi kwa
sababu ya gharama kubwa za matibabu. Wako Wazazi wanakabiliwa na changamoto za
kulea watoto wenye matatizo ya moyo, hawawezi kufanya kazi kama watu wengine
kwa sababu ya uhitaji mkubwa wa huduma kwa watoto wao,” alisema.
Alisema hapa Tanzania kuna
watoto wapatao 750 ambao wako nje wakisubiri kupatiwa matibabu kama hayo lakini
hawawezi kulazwa wote kwa sababu hakuna nafasi ya kutosha. “Tunatamani kujua ni
wapi tutapata mtu wa kutusadia kujenga hilo jengo ili tuweze kuwahudumia watoto
wengi zaidi,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
IJUMAA, JULAI 27,
2018.
No comments:
Post a Comment