HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 28, 2018

WAZIRI MKUU AZINDUA KAMPENI YA KUFUFUA ZAO LA MICHIKICHI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zito Kabwe wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Kigoma kuanza ziara ya kazi mkoani humo Julai 28, 2018.  Wapili kulia ni mkewe Mary na watatu kulia ni Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga. Wapili kushoto ni Mbunge wa Kigoma Kusini, Hasna Mwilima. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 Waziri Mkuu, Kasssim Majaliwa  akizungumza wakati alipoongoza Mkutano wa Wadau wa Michikichi kwenye ukumbi wa NSSF mjini Kigoma Julai 28, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 
*Lengo ni kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini

 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua kampeni ya kufufua zao la michikichi mkoani Kigoma na kuagiza kuanzishwa kwa kituo cha utafiti wa zao hilo katika chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Kihinga kilichopo mkoani Kigoma kwa kuwa ndiko zao la Michikichi linalimwa kwa wingi.

Amesema Serikali imedhamiria kumaliza changamoto ya upatikanaji wa mafuta ya kula nchini kwa kuhamasisha kilimo cha zao la michikichiki kwa sababu kila mwaka Serikali hutumia zaidi ya sh. bilioni 600 kwa ajili ya kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo  (Jumamosi, Julai 28, 2018) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Kigoma, wadau wa zao la michikichi na wabunge wa mkoa wa Kigoma baada ya kuwasili mkoani hapa kwa ziara ya kikazi ya siku nne inayolenga kuhamasisha maendeleo na kilimo cha zao la Michikichi.

Amesema Serikali haiwezi ikaendelea kutumia fedha nyingi za kigeni kuagiza mafuta ya kula kutoka nje wakati uwezo wa kulima michikichi na kuzalisha mafuta ya mawese kwa wingi tunao, hivyo amewataka viongozi wa Serikali wabadilike na wawafuate wakulima kwenye maeneo ya vijijini na wakawasimamie na kuwashauri namna bora ya kulima zao hilo.

Aidha, ameagiza Wizara ya Kilimo ianze taratibu za kisheria za kukihamisha chuo cha Kihinga kutoka Wizara ya Elimu Sayansi ya Teknolojia kwenda wizara ya Kilimo ili shughuli za tafiti za zao la michikichi lifanyike kwa ufanisi. 

Pia, ameiagiza Wizara ya Kilimo kuwahamishia mkoani Kigoma watumishi wa kituo cha utafiti wa michikichi cha Bagamoyo ifikapo mwezi Agosti, 2018 isipokuwa wale wanaohusika na utafiti wa zao la minazi tu.

Kadhalika, amewataka viongozi  wa mikoa yote inayolima michikichi waanzishe mashamba ya michikichiki ili waoneshe mfano kwa wananchi. “Serikali inataka kuona mabadiliko kwenye zao hili. Sioni umuhimu wa Taifa kuendelea kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi wakati uwezo wa kuzalisha ndani upo,”.

Amesema Serikali inataka kuona mabadiliko ya zao hilo, hivyo amewaagiza maafisa ugani katika maeneo yote wanayolima zao hilo wakafualitie maendeleo ya zao hilo kwa ukaribu zaidi. Zao hili litasimamiwa kuanzia hatua za uandalizi wa mashamba, upatikanaji wa pembejeo na utafutaji wa masoko.

Waziri Mkuu amewataka wananchi wote wa mkoa wa Kigoma pamoja na mikoa mingine inayolima michikichi, wahakikishe wanapanda michikichi kwa wingi kuanzia kwenye makazi yao na kwenye mashamba yote wanayolima mazao mengine ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

“Serikali imefanya maamuzi ya kumaliza tatizo la mafuta ya kula nchini, kila mmoja lazima awajibike katika kuinua zao la michikichi ili tuweze kuzalisha mafuta ya kutosha,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Serikali itafuatilia kwa umakini kuhakikisha zao la michikichi linalimwa kwa wingi na kuleta tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla. “Tutumie zao hili kama fursa ya kujikwamua na umasikini pamoja na maliza changamoto ya upatikanaji wa mafuta nchini,”.

AwaliNaibu Waziri wa Kilimo, Bw. Omary Mgumba alisema zao la mchikichiki ni muhimu katika ukuzaji wa uchumi wa nchini, hivyo ufufuaji wa zao hilo ni kichocheo cha viwanda kwa kuwa kutakuwa na uhakika wa upatikanaji wa malighafi, hivyo kuvutia wawekezaji.

Amesema kiasi kikubwa cha zao hilo hutumika katika kuzalisha mafuta ya kula, sabuni, hivyo ameshauri kiwepo chuo cha utafiti wa zao la michikichi mkoani Kigoma ili kurahisisha shughuli za uzalishaji. Mafuta yatokanayo na zao la michikichi yana mahitaji makubwa kwa kuwa bei yake ni nafuu jambo linalowezesha watu wengi wakiwemo wa hali ya chini kuyatumia.

Kwa upande,wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga aliishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kufufua zao la michikichi kwa kuwa linalenga kuinua uchumi wa Taifa.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Mke wa Waziri Mkuu Mary Majaliwa, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhadisi Hamad Masauni, Naibu Waziri wa Ujenzi, uchukuzi na Miundombinu, Mhandisi Atashasta Nditie, Naiubu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, Naibu Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Jpsephat Kandege, Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JULAI 28, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages