*Yasema wasipojirekebisha italivunja baraza lao
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku 30 kwa Madiwani wa Halmashauri ya
Manispaa ya Kigoma Ujiji kujirekebisha na kumaliza tofauti zao ndani ya
siku 30 na iwapo wataendelea na vurugu Serikali haitosita kuvunja baraza
la Madiwani.
Amesema
hatua hiyo inatokana na Madiwani hao kutumia muda mwingi wakigombana
badala ya kuwahudumia wananchi, Serikali inataka kuona wananchi
wakihudumiwa kwa kuboreshewa maendeleo katika maeneo yao na si
kushuhudia viongozi wakigombana kwa maslahi binafsi.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Julai 28, 2018) wakati
akizungumza na wananchi wa mkoa wa Kigoma katika mkutano wa hadhara
uliofanyika Manispaa ya Kigoma Ujiji kwenye uwanja wa Kawawa, akiwa
katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Kigoma.
“Serikali
hairidhishwi na utendaji wenu na nimewapa muda wa mwezi mmoja kumaliza
tofauti zenu. Nataka muendelee kufanya kazi za kuwatumikia wananchi wa
Manispaa hii ambao wamewachagua ili muwatatulie kero zao na si
kuendeleza migogoro,” amesisiza.
Amesema
Madiwani hao wanatakiwa kufuatilia changamoto zinazowakabili wananchi
wao ikiwemo ya upatikanaji wa dawa katika hospitali, zahanati na vituo
vya afya, ambapo licha ya Serikali kutoa fedha nyingi kwa ajili ya
ununuzi wa dawa lakini bado wananchi wanaendelea kukosa huduma hiyo.
Waziri
Mkuu amesema matatizo ya madiwani wa Manispaa hiyo anayafahamu na iwapo
watashindwa kujirekebisha Serikali haitosita kulivunja baraza hilo kwa
sababu Madiwani wake wanatumia muda mwingi kugombana badala ya
kuwahudumia wananchi.
Katika hatua nyingine,Waziri
Mkuu amewahakikishia wananchi wa mkoa wa Kigoma kwamba Serikali
itaboresha miundombinu ya mkoa huo ikiwemo ya reli, barabara, ujenzi wa
bandari na uwanja wa ndege utakaokuwa na uwezo wa kutua ndege kubwa.
Amesema
lengo la maboresho hayo ni kuufanya mkoa huo kuwa kitovu cha biashara
utakaounganisha nchi za Rwanda, Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC)
na Burundi kwa kuimarisha vivutio vya uwekezaji.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JULAI 28, 2018.
No comments:
Post a Comment