*Asema madeni yaliyohakikiwa yamefikia sh. bilioni
127
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali
imelipa sh. bilioni 43 zikiwa ni madeni kwa watumishi wa umma na kati ya hizo
sh. bilioni 16.25 zimelipwa kwa walimu.
“Hadi kufikia mwisho wa mwezi uliopita, jumla
ya sh. bilioni 43 zimelipwa kwa watumishi 27,389 ambao kati yao watumishi
15,919 ni wa sekta ya elimu tu na madeni yao yanafikia sh. bilioni 16.25,”
amesema.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Julai 13, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga akiwa
aktika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
“Mapema mwaka huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi kutoa sh. bilioni 200 za
kulipa madeni ya watumishi na hadi sasa madeni ambayo yameshahakikiwa ni sh.
bilioni 127 na mengine ni ya wazabuni,” amesema.
Amesema hivi sasa Serikali inadhibiti uzalishaji wa
madeni ya watumishi kwa kuzuia uhamisho kama hakuna fedha, kuzuia rufaa zisizokuwa
za lazima na ambazo hazina ufuatiliaji wa waganga wakuu wa mikoa na wilaya, na
kuhimiza matumizi ya Bima ya Afya kwa watumishi wa umma.
“Mkurugenzi kama hakikisha unampa mtumishi barua ya
uhamisho kama fedha ipo, na kama hakuna fedha umpe barua inayosema utamlipa
lini fedha yake ya uhamisho. Kwenye matibabu, DMO hakikisha unawasiliana na
daktari mahsusi wa hospitali ambako mtmishi wako amepewa rufaa aende, pia
fuatilia matibabu yake ni ya siku ngapi ili akimaliza arudi kwenye kituo chake
cha kazi, siyo abaki kula raha mjini tu,” amesema.
Wakati huohuo, Naibu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bw. Joseph Kakunda amesema Serikali
itakamilisha uratibu wa ajira za walimu 16,040 ifikapo Julai 16, mwaka huu.
“Kati ya hao, walimu 10,030 watapelekewa shule
za msingi na walimu 6,010 watapangiwa shule za sekondari. Wale wote wenye nia
ya kufanya kazi ya ualimu walete maombi yao kabla ya tarehe 16 Julai, wasikae
nyumbani wakifikiri kuwa kazi zitawafuata, tunaajiri watumishi wenye kuonyesha
nia ya kufanya kazi,” alisema.
Naye Mbunge wa Kishapu,
Bw. Selemani Nchambis alisema anaiomba Serikali isaidie kuwapatia sh. milioni
250 kwa ajili ya kukamilisha kazi ya usambazaji maji kwenye mji wa Maganzo.
Tunashukuru kwa kupatiwa mradi wa maji ya
kutoka Ziwa Victoria, tumeshalaza mabomba umbali wa km.25 lakini tunahitaji sh.
milioni 250 za kukamilisha mradi. Mji wa Maganzo ni wa siku nyingi, na una
historia kubwa. Tunaamini Serikali itasikia kilio chetu,” alisema.
Pia aliomba ijengwe barabara ya lami ya km.48
kutoka njia panda ya Shinynga hadi kituo cha afya cha Kishapu ili kuwaepusha
akinamama na adha wanazozipata pindi wakizidiwa.
Mapema,
akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na watumishi hao, Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga, Bibi Zainab Tallack alisema uuzaji wa zao la pamba kwenye mkoa huo
unaendelea vizuri na kwamba hadi sasa wameshauza kilo 3,319,823.9 na nyingine
ziko kwenye maghala na nyingine bado ziko shambani.
“Tulipoanza msimu tulitarajia kuwa na wakulima
28,540 lakini sasa hivi tunao wakulima 44,088 na tunatarajia kuvuna tani
77,197,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, JULAI 13, 2018.
No comments:
Post a Comment