HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 30, 2018

NIMERIDHISHWA NA HATUA ZA AWALI ZA UWEKEZAJI MKINGA-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Tanga, Henry Shekifu wakati alipowasili kwenye uwanja wa Ndege wa Tanga kuanza ziara  ya kazi mkoani humo, Oktoba 30, 2018. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
  Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela wakati alipowasili kwenye uwanja wa Ndege wa Tanga kuanza  ziara ya  kazi mkoani humo Oktoba 30, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

 Tanga, Tanzania

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea eneo la mradi wa ujenzi wa viwanda 11 katika kijiji cha Mtimbwani wilayani Mkinga, ambapo amesema ameridhishwa na hatua za awali za uwekezaji huo.

Katika eneo hilo vinatarajiwa kujengwa viwanda mbalimbali kikiwemo cha saruji cha Hengya, kiwanda cha vioo, kiwanda cha vifaa vya kisasa vya ujenzi, uzalishaji wa umeme kwa kutumia makaa ya mawe.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Oktoba 30, 2018) wakati akizungumza na wananchi katika kijiji cha Mtimbwani wilayani Mkinga akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Tanga.

Amesema uwekezaji huo unatarajiwa kulinufaisha Taifa na wananchi wakazi wa wilaya ya Mkinga kwa kuwa kinatarajiwa kuajiri zaidi ya watu 8,000, hivyo amewaomba wananchi hao waendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji hao.

Kuhusu wananchi ambao eneo lao limechukuliwa na wawekezaji na bado hawajalipwa fidia Waziri Mkuu amewataka wawe na subira kwa kuwa wote watalipwa. “Muwekezaji amenihakikishia kwamba atawalipa wananchi wote wanaodai fidia.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuuamewataka watumishi wa umma kutenga siku tatu katika wiki na kuwafuata wananchi waishio maeneo ya vijijini kwa ajili ya kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi.

Amesema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kuwatumikia wananchi bila ya ubaguzi wa kidini, kisiasa, rangi  na kimapato, hivyo amewataka watumishi hao wafanye kazi kwa bidii.

Awali, Mbunge wa jimbo la Mkinga, Dastan Kitandula ameishukuru Serikali kwa niaba ya wananchi wa Mkinga baada ya Serikali kufuta hati ya shamba la moa na kuirudisha ardhi hiyo kwa wananchi, pia ameomba ifute hayi za mashamba mengine yaliyotekelezwa katika Tarafa ya Maramba.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, OKTOBA 30, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages