Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja wa benki hiyo, Tully Mwambapa, wakimpongeza Ofisa Masoko Mwandamizi wa benki hiyo, Ninael Munuo, baada ya kuvutiwa na maelezo aliyoyatoa kwa Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu, kuhusu huduma zitolewazo na benki hiyo ikiwemo SimAccount, wakati wa Wiki ya Maonyesho ya Viwanda Mkoa wa Pwani. (Picha na Francis Dande).
Kibaha, Tanzania
MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid
Nsekela, amesema watendaji benki hiyo wapo tayari kuwahudumia watanzania wote
na kuwashauri juu ya matumizi sahihi ya fedha na huduma za kibenki.
Nsekela alisema hayo Mjini Kibaha juzi wakati wa
uzinduzi wa Maonesho ya Viwanda Mkoa wa Pwani yaliyodhaminiwa na benki hiyo.
Alisema kipindi chote cha maonesho hayo, CRDB
imebeba kaulimbiu ya ‘Tupo Tayari’ ikilenga kutoa huduma na ushauri wa kifedha
kwa watu wote watakaohudhuria maonesho hayo yaliyoanza Oktoba 29
yatakayofanyika hadi Novemba 4 mwaka huu.
Akifafanua maana ya kaulimbiu hiyo mbele ya Makamu
wa Rais, Samia Hassan Suluhu, mkurugenzi mtendaji huyo alisema CRDB wapo tayari
kufanya kazi kwa karibu zaidi na serikali, wafanyabiashara wakubwa wakati,
wadogo na wajasiriamali.
“Maonesho haya yanatupa imani kwamba sekta ya fedha
ni muhimili muhimu kwenye uchumi ndio maana tukaona tuingie tukiamini hapa
tutakutana na wadau wa aina tofauti na tutawahudumia.
“Kwa taarifa tu ni kwamba CRDB ndio benki
inayoongoza kwa kutoa mikopo hapa nchini, tupo pia kwenye sekta ya Kilimo
ambayo ndio mgongo wa viwanda ambavyo tunataka vitupeleke kwenye uchumi wa kati.
…Mwaka huu peke yake kwenye kilimo tumewakopesha
wakulima na tunao mpango wa kuwakopesha wakulima zaidi nchi nzima.
“Mheshimiwa Makamu wa Rais, mikopo tuliyoitoa
kwenye kilimo ni Sh. Bilioni 433.5 sawa na asilimia 15 tu ya mikopo yote
iliyotolewa na benki yetu kwa mwaka huu.
“Hili linaifanya benki yetu ya CRDB kuendelea kuwa
kinara katika utoaji wa mikopo kwenye sekta ya kilimo… lakini pia tumetoa
mikopo ya zaidi ya Sh. Bilioni 57.8 katika biashara na katika sekta ya
usafirishaji ili kurahisha kuyafikia masoko.
“Sisi tunaamini kuwa ili viwanda viweze kushamiri,
ni muhimu sana kusaidia kuongeza uzalishaji ulio na tija, usafirishaji na
kufungua masoko kwenye maeneo mengine.
“Mwaka jana benki yetu ilitoa mikopo ya Sh. Bilioni
11 katika sekta ya uzalishaji yaani ‘Manufacturing’ pamoja na huduma hizo za
mikopo, CRDB pia ina huduma nyingine nyingi kwa ajili ya wenye viwanda,”
alisema Nsekela.
Alizitaja huduma hizo kuwa ni dhamana za biashara, huduma za bima, huduma
za hazina (fedha za kigeni), akaunti ya hundi maalum kwa biashara, mifumo
jadidi ya malipo ambazo ni (Expronet, Internet Banking, SimBanking,
FahariHuduma Wakala), mfumo wa malipo wa Serikali (GePG) na madawati maalum ya
biashara za China na India.
Akizungumzia utayari wa CRDB, Waziri wa Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema amefurahishwa na udhamini wa
benki hiyo kwenye maonesho hayo na kuahidi kuwaeleza wawekezaji huduma bora
zinazotolewa na CRDB.
“Ninakutana na wawekezaji kila kukicha ninawaahidi
CRDB nitakuwa balozi wetu, nitazungumzia huduma zenu ili nao waje muwahudumie.
“Nami nasema hapa nipo tayari kuwaletea wawekezaji
wanaotaka fedha ili muwahudumie,” alisisitiza Waziri Mwijage.
Alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wakazi wa Mkoa wa
Pwani na watanzania wote kuitumia benki ya CRDB na wataalamu wake kwa kupata
ushauri wa masuala ya kifedha hasa mikopo ya kibiashara.
No comments:
Post a Comment