WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya kwenye maeneo
mbalimbali nchini yakiwemo ya halmashauri ya wilaya ya Lushoto.
Amesema
lengo ni kuhakikisha kila kata inakuwa na kituo cha afya chenye uwezo
wa kutoa huduma mbalimbali muhimu zikiwemo za maabara, upasuaji na mama
na mtoto.
Ametoa
kauli hiyo leo (Jumatano, Oktoba 31, 2018) wakati akizungumza na
wakananchi katika kata ya Malindi, baada ya kutembelea jengo la soko
mbogamboga la Malindi.
Waziri
Mkuu amesema Serikali imejipanga vizuri katika sekta ya afya baada ya
bajeti ya kununulia dawa kuongezeka kutoka sh. bilioni 31 kwa mwaka na
kufikia bilioni 269.
“Hatutaki
tena kusikia mgonjwa anaenda hospitali na kukosa dawa biashara hiyo
tumeimaliza, Rais Dkt. John Magufuli ametoa fedha nyingi kwa ajili ya
ununuzi wa dawa.”
Amesema
katika wilaya ya Lushoto Serikali imetenga sh. bilioni 1.4 kwa ajili
ujenzi na ukarabati wa majengo ya vituo vya afya vya kata za Kangagai.
Mnazi na Mlola.
“Halmashauri
wekeni mpango thabiti wa kujenga wodi mbili kati yake moja ya wanaume
na nyingine ya wanawake, lengo la Serikali ni kuboresha huduma za afya
kwa wananchi.”
Aizungumzia
kuhusu mradi wa ujenzi wa soko, Waziri Mkuu amesema mradi huo ni sehemu
ya huduma zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuboresha huduma za
jamii nchini.
Waziri
Mkuu ametaja huduma nyingine zinazotolewa na Serikali kwa wananchi ni
za afya, elimu, maji, uchumi na ujenzi na uboreshwaji miundombinu
mbalimbali ikiwemo ya barabara.
Hivyo,
amewataka wananchi watumie vizuri soko hilo ambalo linatoa fursa kwao
kufanya biashara katika eneo zuri na kuwawezesha kuuza bidhaa zao zikiwa
katika ubora.
Pia
amewashauri wakulima hao wajiunge katika vikundi na kuanzisha ushirika
wao ili waweze kusaidiwa na Serikali katika kupata mikopo kwa ajili ya
kuzalisha kwa ubora zaidi.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Lushoto, Bibi Ikupa Mwasyoge
amesema kukamilika kwa soko hilo kutainufaisha halmashauri na wananchi.
Bibi.
Ikupa amesema ujenzi wa jengo hilo la soko la ghorofa mbili
lililojengwa kwa awamu mbili ulianza mwaka 2011 na umekamilika Septemba
2018, umegharimu sh. bilioni 1.1.
Amesema
halmashauri itanufaika kwa kupata ushuru na wananchi ambao wengi wao ni
wakulima wa mboga na matunda watakuwa na sehemu ya uhakika wa kufanyia
biashara.
“Wakulima
35,000 wa kata ya Malindi na kata jirani za Lukozi, Manolo na Shume
wanaozalisha wastani wa tani 5,900 za mboga na matunda kwa mwaka
watanufaika.”
Naye,
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu amesema Serikali imefanya kazi kubwa katika kuboresha huduma za
afya nchini.
Amesema
bajeti ya dawa katika halmashauri hiyo imeongezeka kutoka sh milioni
183 za dawa zilizokuwa zinatolewa awani na sasa imefikia sh milioni 565.
Mbunge
wa jimbo la Mlalo, Bw. Rashid Shangazi ametumia fursa hiyo kuishukuru
Serikali kwa kuwasaidia wananchi wa halmashauri kuongeza thamani ya
mazao yao kabla ya kuuza.
Awali,Waziri
Mkuu alizindua jengo la utawala la Halmashauri ya wilaya ya Lushoto
lililogharimu sh. bilioni 4.3. Kukamilika kwa jengo hilo kutaboresha
huduma kwa wananchi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, OKTOBA 31, 2018.
No comments:
Post a Comment