HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 28, 2018

SERIKALI YAWAPONGEZA WANUFAIKA WA MIRADI YA MAENDELEO KWA KUTUMIA VIZURI FEDHA ZA MIRADI WANAZOZIPATA KWA KUTEKELEZA SERA YA UCHUMI WA VIWANDA NA KUJIKWAMUA KIUCHUMI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) akiangalia moja ya bidhaa iliyotengenezwa na mnufaika wa Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) wa kikundi cha Pamoja, kata ya Gangilonga mkoani Iringa wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo yenye lengo la kuzungumza na watumishi wa umma na kutembelea miradi inayotekelezwa na taasisi zilizo chini ya ofisi yake.Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) akipata maelezo ya bidhaa zilizotengenezwa na wanufaika wa Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) wa kikundi cha Maridadi, kata ya Kihesa mkoani Iringa wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo yenye lengo la kuzungumza na watumishi wa umma na kutembelea miradi inayotekelezwa na taasisi zilizo chini ya ofisi yake.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) akikabidhi hati ya umiliki wa ardhi kwa mmoja wa wanufaika wa mradi wa MKURABITA, kata ya Igumbilo mkoani Iringa wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo yenye lengo la kuzungumza na watumishi wa umma na  kutembelea miradi inayotekelezwa na taasisi zilizo chini ya ofisi yake.

 Iringa, Tanzania
Serikali imewapongeza wanufaika wa miradi ya maendeleo mkoani Iringa hususani akina mama kwa kutumia vizuri fedha za miradi ya maendeleo wanazozipata kwa kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwa ni hatua ya utekelezaji  wa sera ya uchumi wa viwanda.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) wakati akikagua miradi ya maendeleo ya Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF), Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) katika kata za Gangilonga, Kihesa na Igumbilo mkoani Iringa.
Mhe. Mkuchika amesema, fedha za miradi zimekuwa zikitolewa kwa akina mama na vijana lakini akina mama wamekuwa wakijiongeza zaidi kwa kidogo wanachokipata na kufanya mambo ya maendeleo kama vile ufugaji, ushonaji, usindikaji wa vyakula, ujenzi wa nyumba, kununua sare za shule za watoto, shajala na kufanya mambo mengine ya maendeleo yanayowawezesha kujikwamua kiuchumi.
“Nawapongeza sana akina mama kwani pamoja na fedha kidogo za miradi mnazozipata lakini mmekuwa mkifanya shughuli mbalimbali za ujasiliamali na kuongeza thamani ya bidhaa mnazozalisha  ambazo zinawaongezea kipato mambo.” Mhe. Mkuchika ameongeza.
Aidha, Mhe. Mkuchika amewataka vijana nchini kuiga mfano wa akina mama wanavyojishughulisha na masuala ya ujasiliamali ili waweze kubadilisha maisha yao na kuwa na tija kwa maendeleo ya taifa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mkuchika amekabidhi hati tatu (3) za umiliki wa ardhi kwa wananchi wa Kata ya Igumbilo, hati hizo ni miongoni mwa hati 59 zilizo  tayari kukabidhiwa kwa wananchi wa kata hiyo ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Urasimishaji Ardhi Manispaa ya Iringa.
Ameongeza kuwa Serikali imerahisisha utoaji wa hati hizo za umiliki wa ardhi kupitia MKURABITA ili wananchi waweze kupata fursa ya kukopa katika taasisi za kifedha kwani hati hizo zinatambulika kisheria.
Mhe. Mkuchika amewasifu wakazi wa kata hiyo kwa hatua nzuri ya urasimishaji wa ardhi kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia mali zao kutambuliwa na kuwawezesha kupata mitaji kupitia mikopo hiyo.
Jumla ya viwanja 1,287 vimepimwa katika kata ya Igumbilo mitaa ya Mlangali na Igumbilo kupitia utekelezaji wa mradi wa MKURABITA.
Mhe. Mkuchika yuko mkoani Iringa kwa ziara ya siku mbili ya kikazi yenye lengo la kuzungumza na Watumishi wa Umma na kutembelea utekelezaji wa miradi ya Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF), Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) ambapo ameweza kujionea shughuli mbalimbali za maendeleo zinazotekelezwa na wanufaika wa miradi hiyo.
IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS (UTUMISHI)
TAREHE 28 OKTOBA, 2018

No comments:

Post a Comment

Pages