Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H.
Mkuchika (Mb) akizungumza na watumishi wa umma wilayani Kilolo wakati wa ziara
yake ya kikazi mkoani Iringa yenye lengo la kuwasikiliza, kupokea changamoto
zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi ili kuboresha utumishi wa umma na
kuongeza tija katika kuwahudumia wananchi.
Baadhi ya watumishi
wa umma wilayani Kilolo wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb)
(hayupo pichani) wakati akizungumza nao kwa lengo la kuwasikiliza, kupokea
changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi ili kuboresha utumishi wa
umma na kuongeza tija katika kuwahudumia wananchi.
Iringa, Tanzania
Iringa, Tanzania
Serikali imewataka Watumishi
wa Umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa kuishi maeneo
wanayofanyia kazi yaani katika wilaya hiyo kwa lengo la kutekeleza majukumu yao
ipasavyo.
Kauli hiyo
imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George
H. Mkuchika (Mb) wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Kilolo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi katika mkoa wa Iringa.
Mhe. Mkuchika
amesema kuna baadhi ya watumishi wameajiriwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo
lakini wanaishi Iringa mjini jambo ambalo ni kinyume na taratibu za kiutumishi
na pia linasababisha watumishi hao kutokuwa makini katika utendaji kazi wao.
Mhe. Mkuchika amemuagiza
Mkuu wa Wilaya ya Kilolo kuhakikisha ifikapo Januari, 2019 wote wawe
wameshahamishia makazi yao katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo na asiyefanya
hivyo atakuwa amejifukuzisha kazi.
“Ninatoa muda wa miezi
miwili kwa watumishi hao kuweka makazi yao Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo
haraka iwezekanavyo na asiyetaka aandike barua ya kuacha kazi,” Mhe. Mkuchika
amesisitiza.
Mhe. Mkuchika
ameongeza kuwa lengo la Serikali la kutaka Kilolo kuwa Makao Makuu ya
Halmashauri ni kuwawezesha wananchi kupata huduma bora na kwa wakati.
Mhe. Mkuchika
amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Iringa ambayo ililenga kuzungumza na
watumishi wa umma, kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuzitafutia
ufumbuzi, pamoja na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na taasisi
zilizo chini ya ofisi yake.
IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS (UTUMISHI)
TAREHE 28 OKTOBA,
2018
No comments:
Post a Comment