TANGU
Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani chini ya uongozi wa
Rais Dk. John Magufuli, imekuwa ikitilia mkazo ukusanyaji kodi kupitia
vyanzo mbalimbali vya serikali.
Mapato
ya kodi yanayokusanywa yamewezesha Serikali kugharamia miradi mikubwa
ya kiuchumi iliyopo kwenye mkakati wa kuliwezesha Taifa kufikia uchumi
wa viwanda.
Hata
hivyo licha ya jitihada hizo ukwepaji wa kodi na biashara za magendo
zinayofanywa na baadhi ya wafanyabiashara kwa kushirikiana na watumishi
wa umma wasiokuwa waaminifu mipakani, wamelifanya Taifa limekuwa
linapoteza mapato yatokanayo na kodi.
Serikali
mara kwa mara kupitia vyombo vya dola imekuwa ikiendesha msako
kuwakamata watu wanaokwepa kodi na kuwafikisha katika vyombo vya sharia.
Cha
kustaajabisha baadhi ya askari waliopewa dhamana hiyo ndiyo
wanashirikiana na wafanyabiashara katika kusindikiza bidhaa za magendo.
Hali hiyo imebainika mwezi huu wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alipokuwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Kagera.
Waziri
Mkuu alibaini kuwepo kwa baadhi ya askari polisi pamoja na watumishi wa
forodha kwenye mipaka Tanzania na nchi za Uganda na Rwanda, wakishiriki
kuvusha magendo.
Jambo
hilo la kusikitisha lilionyesha kumkera Waziri Mkuu, hivyo kuwaagiza
viongozi wa mkoa huo kuhakikisha wanaongeza umakini katika usimamizi wa
mipaka hususan kwa watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Jumapili,
Oktoba 7 mwaka huu, baada ya kukagua kiwanda cha kukoboa kahawa cha
Nkwenda wilaya Kyerwa, Waziri Mkuu alimuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kagera, Augustine Olomi, awachukulie hatua askari polisi wote wa wilaya
ya Kyerwa wanaotuhumiwa kusindikiza kahawa ya magendo inayouzwa nchi
jirani. Miongoni mwa polisi hao yupo aliyekuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya
hiyo, Justin Joseph.
“Askari
polisi wa wilaya ya Kyerwa pamoja na OCD wao wanatuhumiwa kusindikiza
kahawa inayosafirishwa kwa njia ya magendo kwenda nchi ya jirani kupitia
njia mbalimbali zisizo rasmi zikiwemo za Kumisongo, Kashaijo na
Omukatoma.” alibanisha.
Waziri
Mkuu alisema ni jambo la hatari kama askari polisi wanasindikiza kahawa
inayouzwa kwa magendo, hivyo ameagiza jambo hilo lidhibitiwe haraka.
"Marufuku kupeleka kahawa nje ya nchi kwa njia ya magendo na polisi
msishiriki katika butura.” alitoa msisitizo.
Katika
kuonesha kuwa Serikali imekerwa na vitendo hivyo vya polisi kujihusisha
na biashara za magendo, ikiwemo kusindikiza kahawa inayosafirishwa
kwenda nchi jirani kwa njia hiyo, Rais Dk. Magufuli, Oktoba 8, mwaka huu
aliagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kagera, Augustine Olomi.
Askari
wengine alioagiza wasimamishwe kazi ni Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya
Kyerwa, Justin Joseph, Mkuu wa Upelelezi wa wilaya ya Kyerwa, Evererist
Kivuyo na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Kyerwa, Robert Marwa.
Viongozi
hao wamesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za kuhusika
katika magendo ya zao la kahawa katika wilaya ya Kyerwa pamoja na tuhuma
nyingine.
Waziri
Mkuu alisema kuna askari polisi wa wilaya hiyo walikwenda kufanya kikao
na wafanyabiashara wa nchi jirani na kupanga mikakati ya kuvusha bidhaa
mbalimbali ikiwemo kahawa kwa njia ya magendo ambapo walipewa ng’ombe
wawili.
Alisema
mbali na askari polisi pia, baadhi ya watumishi wa idara ya forodha nao
wanatuhumiwa kujihusisha na biashara ya magendo hususan katika mipaka
ya Mulongo na Mutukura.
Baada
ya kuchukizwa na biashara za magendo zinazofanywa na baadhi ya
watumishi katika wilaya hiyo ya Kyerwa, Oktoba 10 mwaka huu, Waziri Mkuu
aliwataka viongozi wa wilaya hiyo wajipime.
Alisema
Serikali imewapeleka katika wilaya ya Kyerwa ili wakafanye kazi kwa
kuzingatia maadili ya utumishi na si vinginevyo na kwamba watumishi wote
watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao hawana nafasi katika awamu hii.
Pia,
Waziri Mkuu alimuagiza Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa
wa Kagera, Adam Ntogha, kumsimamisha kazi Ofisa wa Forodha katika mpaka
wa Mulongo, Peter Mtei kwa tuhuma za kujihusisha na biashara za magendo.
“Biashara
za magendo zinafanyika bila ya wao kuchukua hatua, mnatia aibu yaani
hakuna kazi inayofanyika. Viongozi wa wilaya ya Kyerwa mjipime wenyewe,
mialo mingi katika wilaya yenu inatumika kwa biashara ya magendo na
butura.”
Aliongeza
kuwa katika mwalo wa Mulongo ulipo kwenye eneo ambalo Tanzania
inapakana na nchi za Uganda na Rwanda, biashara za magendo na butura
zinafanyika na hakuna kiongozi wanaochukua hatua.
Waziri
Mkuu alimtaka Meneja wa TRA asiwahamishe watumishi wabovu kutoka kituo
kimoja cha forodha na kuwapeleka kingine kwa kuwa huko anakowapeleka
wanakwenda kuendeleza biashara za magendo na kuikosesha Serikali mapato.
Alitolea
mfano mtumishi wa mamlaka hiyo, Mtei ambaye alihamishiwa kituo cha
Mulongo akitokea kwenye kituo cha Mtukura kilichopo katika mpaka wa
Tanzania na Uganda kwa tuhuma za kuchua rushwa na kushirikiana na
wafanyabiashara wa butura.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu alisema mtumishi huyo tayari alishapewa barua ya
uhamisho kwenda katika kituo cha forodha cha Rusumo miezi minne
iliyopita hadi sasa hajahama na anaendelea na biashara za magendo ambapo
Agosti 5, mwaka huu anadaiwa kupitisha mzigo wa magendo uliobebwa
kwenye gari aina ya fuso yenye za usajili T 957 AXF mali ya Erasto Muga.
“Meneja
TRA msimamishe kazi Mtei, hatuwezi kuwa na watumishi wabovu alafu nyie
mnawahamisha vituo ili wakaendelee kuharibu eneo lingine. Mnajua mkakati
wa Serikali hii ni kudhibiti rushwa hivyo hatuwezi kuvumilia suala
hili.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu alimuagiza Meneja wa TRA wa mkoa wa Kagera afanye ukaguzi
kwenye vituo vyote vya forodha katika mkoa huo pamoja na kuongeza idadi
ya watumishi na kudhibiti vitendo vya rushwa.
Biashara
ya magendo kwa muda mrefu imekuwa ikiikosesha Serikali mapato kwa kuwa
fedha zinazotakiwa kulipwa kodi na kuingia kwenye mfuko wa Serikali
zimekuwa zikiishia mikononi mwa watendaji wasiokuwa waaminifu.
Jambo
hilo kwa kiasi kikubwa limekuwa likirudisha nyuma mipango ya Serikali
ya kuwaletea wananchi maendeleo kama uboreshaji wa huduma za jamii na
ujenzi wa miundombinu.
Wananchi
pamoja na wafanyabiashara wanatakiwa watambue kuwa wanawajibu wa kulipa
kodi na kwamba tayari Serikali imeshatoa maelekezo kwa Jeshi la polisi
kuwakamata wote wanaokwepa kodi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, OKTOBA 29, 2018.
No comments:
Post a Comment