Mkurugenzi wa Kampuni ya Trumark inayojishughulisha na masula ya vijana, Agnes Mgongo akizungumza wakati wa mkutano na viongozi wa Klabu za Jogging Mkoa wa Dar es Salaam uliohusu kutathmini maandalizi ya Tamasha la Wezesha Sport Tanzania litakalofanyika Desemba 2 mwaka huu.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Trumark, Agnes Mgongo akizungumza katika mkutano huo.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Trumark, Agness akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa KIJA, Ahmad Mussa.
Katibu wa Chama Cha Jogging Wilaya ya Kinondoni (KIJA) ,Alhaji Seif Muhere, akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Trumark, Agnes Mgongo.
Mkutano ukiendelea.
Wenyeviti na Makatibu wa Jogging Klabu za wilaya tano za Jiji la Dar es Salaam pamoja na wakurugenzi wa Kampuni za Trumark, Agnes Mgongo na Elizabeth Masaba wa On Fitnes wakiwa kwenye kikao hicho.
Na Kulwa Mwaibale
MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Trumark, Agnes Mgongo amekutana na viongozi wa Klabu za Jogging za Mkoa wa Dar es Salaam na kufanya nao mazungumzo kutathmini maandalizi ya Tamasha la Wezesha Sport Tanzania linalotarajiwa kufanyika Desemba 2 mwaka huu katika Viwanja vya Posta Kijitonyama.
Akizungumzia tamasha hilo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kampuni ya Power On Fitnes, Elizabeth Masaba ambaye wameandaa pamoja tamasha hilo, Mgongo alisema lengo lao ni kuhamasisha jamii kufanya kazi au biashara kwa ufanisi na kuwaburudisha.
"Nilikaa na mwenzangu Masaba tukajadiliana namna tunavyoweza kuwakusanya watu kwa wingi ili tuwahamasishe kufanya kazi zao kwa ufanisi ndipo tukaona tufanye tamasha hili la Wezesha Sport Tanzania," alisema Mgongo.
Mgongo ametoa rai kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kwenye tamasha hilo ambalo litawaacha wakiwa wamenufaika kwa mengi.
Aliongeza kuwa licha ya kuwahamasisha kuhusu suala la ufanisi kwenye maeneo yao ya kazi watapata burudani kupitia michezo mbalimbali ya jogging, mpira wa miguu, pete, kuvuta kamba, kukimbiza kuku, muziki na mingine mingi.
Katika hatua nyingine viongozi wa kalabu hizo wametoa kilio chao kwa serikali iwaunge mkono kama inavyofanya kwenye michezo mingine.
Kilio hicho kimetolewa na Katibu wa Chama cha Jogging Wilaya Kinondoni (KIJA), Alhaji Seif Muhere ambao ni wenyeji wa tamasha hilo katika kikao cha viongozi wa jogging wa wilaya tano za jijini Dar es Salaam pamoja na wakurugenzi wa Kampuni ya Trumark, Agnes Mgongo na Elizabeth Masaba wa Power On Fitnes.
Kikao hicho kilichofanyika mwishoni mwa wiki kilikuwa mahususi kwa ajili ya kufanya tathmini ya maandalizi ya tamasha hilo.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Muhere alisema kama serikali itavitazama vikundi vya jogging na kuvisaidia, vinaweza kufanya mambo mengi ya kimaendeleo.
"Serikali ikivisapoti vikundi vya jogging kama inavyofanya kwenye michezo mingine, vitafanya mambo makubwa ya kimaendeleo kama kuanzisha viwanda vidogo na biashara mbalimbali," alisema Muhere.
Muhere ametoa kilio chake kwa serikali kuwasaidia kwani vikundi vingi vya joggig havina vifaa vya michezo kama jezi na mitaji ya kufanya shughuli za kimaendeleo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Jogging Wilaya ya Kinondoni, Ahmad Mussa alisema, kwa kuwa kwenye vikundi vya jogging kuna wataaluma kama madaktari, walimu, wahandisi, askari na wengine wengi kwa kushirikiana nao wanaweza kufanya shughuli za kimaendeleo zitakazoliingizia fedha taifa kupitia kodi.
No comments:
Post a Comment