*Aagiza fedha zilizotengwa zikatumike katika kujengea hospitali Dodoma
Rais
Dkt. John Pombe Magufuli ameahirisha maadhimisho ya siku ya Uhuru,
Disemba 9, 2018 na fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha
shamrashamra hizo ameelekeza zitumike kujenga hospitali mkoani Dodoma
ambayo itaitwa Uhuru Hospitali.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa leo (Jumanne, Novemba 20, 2018) na Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, Rais Dkt. Magufuli ameagiza kiasi cha shilingi
milioni 995.182 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha sherehe
hizo zitumike kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mkoani Dodoma.
Waziri
Mkuu ametoa taarifa hiyo wakati alipokutana na viongozi waandamizi wa
mkoa wa Lindi pamoja na wilaya zake katika kikao cha maandalizi ya
shughuli za kuzima Mwenge kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano
kwenye ofisi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Amesema
hospitali hiyo itakayojengwa katika eneo la kati ya barabara ya kwenda
Hombolo na Chamwino kwenye barabara ya kwenda Dar es Salaam itakuwa
inawahudumia wakazi wa mkoa wa Dodoma pamoja na wananchi wengine
watakaokuwa mkoani humo.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli amewaagiza wakuu wa mikoa na
wilaya waandae matukio watakayoyatekeleza katika maeneo yao
yatakayoashiria maadhimisho ya siku ya Uhuru. “Wanaweza kutumia siku
hiyo kwa kufanya usafi maeneo ya wazi au kwenye hospitali.”
Kufuatia
maagizo hayo, Waziri Mkuu amewataka wananchi katika maeneo yote nchini
wajiandae kufanya shughuli mbalimbali za kijamii zitakazopangwa na wakuu
wao wa mikoa na wilaya kufanyika katika maeneo yao.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, NOVEMBA 20, 2018.
No comments:
Post a Comment