HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 13, 2019

MAIGE AANZA KUPIGIA DEBE KISWAHILI KITUMIKE KATIKA UFUNDISHAJI KWENYE SEKONDARI

Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini, Almas Maige, akiwaonyesha waandishi wa habari vitabu vya masomo mbalimbali ambavyo vimeshaandaliwa kwa ajili ya kufundishia sekondari kwa lugha ya kiswahili kama hoja ya mtumizi ya kiswahili katika kufundishia na kujifunza itapitishwa na Bunge.
 
NA TIGANYA VINCENT, TABORA

MBUNGE wa Jimbo la Tabora Kaskazini Almas Maige amesema wakati umefika wa Watanzania kuanza kutumia lugha ya Kiswahili kwa ajili ya kufundishia katika shule za Sekondari na Vyuo vya Ufundishaji wa masomo yote.

Hatua itasaidia kuwawezesha vijana wengine kuelewa wanachofundishwa na kuwa na ufanisi katika utendaji kazi.

Maige alisema hayo jana mjini Tabora wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya Hoja yake aliyoipeleka Bunge ya kutaka Kiswahili kitumike lugha ya kifundishia na kujifunza katika Shule ya Sekondari ya Vyuo hapa nchini.

Alisema utafiti uliofanywa na wataalamu na wanazuoni mbalimbali umeonyesha kuwa asilimia 50 ya wanafunzi hawaelewi wanachofundishwa kutoka na matumizi ya lugha ya kiingereza.

Maige aliongeza kuwa hata wanavyuo vya ufundi wanaofundishwa kwa lugha ya kiingereza wanapomaliza masomo yao wanapokuwa kazini hawatumii lugha hiyo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku bali wanatumia Kiswahili.

Mbunge huyo wa Jimbo la Tabora Kaskazini alisema kuwa tayari maandalizi ya vitabu vya kufundishia Kidato cha Kwanza kwa masomo yote vimekamilika pamoja na Kamusi kubwa ya tafsiri wa maeneo yote ya Kiswahili iko tayari.

Aliongeza kuwa wataalamu walioandika vitabu hivyo wanasema ikiwa Kiswahili kitaanza kutumia wako tayari kuandaa na vitabu vya Kidato cha Pili na kuendelea kwa muda mfupi na wanafunzi waanze kuvitumia.

Maige alisisitiza kuwa kwa juhudi hizo za wataalamu hakuna sababu ya kuendelea kutumia lugha ambayo baadhi ya wanafunzi hawaelewi wanachofundishwa.

Alisema kuwa hata wananchi wamekuwa wakizielewa zaidi hotuba za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na mijadala ya vikao vya Bunge kwa sababu ya matumizi ya Kiswahili.

Maige alisisitiza kuwa wakati umefika wa kumuunga mkono Rais Magufuli kwa moyo wake aliouonyesha wa kukiimarisha Kiswahili ndani na nje ya Tanzania wakati akihutubia mikutano mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Pages