HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 13, 2019

RAS TABORA AAGIZA WAKUU WA IDARA KUTOA MAFUNZO KUHUSU HAKI ZA BINADAMU KWA WALIOCHINI YAO

NA TIGANYA VINCENT, TABORA

WAKUU wa Idara wa Halamshauri zote za Mkoani Tabora wametakiwa kuhakikisha wanawajengea uwezo kuhusu masuala ya haki za binadamu na upatikanaji wa haki kisheria watumishi waliochini yao ili wasaidie kuieneza katika maeneo wanayosimamia.

Hatua itasaidia kupeleka elimu hiyo kwa watu wengi hadi ngazi za vijiji na familia ambapo kuna maeneo ambayo yana uvunjifu wa haki za binadamu na upatikanaji wa haki za kisheria na kuwezesha wananchi kupata huduma nzuri.

Kauli hiyo imetolewa juzi mjini hapa na Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu wakati akifungua mafunzo ya watumishi wa Serikali za Mitaa ambao wanaoandaliwa kuwa wakufunzi wa masuala kuhusu haki za binadamu na upatikanaji wa haki za kisheria yaliyoandaliwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Alisema kuwa utekelezaji wa haki za binadamu hapa mkoani Tabora bado unakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo mauaji ya vikongwe kwa imani za kishirikina na yale yanayotokana na wivu wa mapenzi.

Makungu aliongeza kuwa uelewa wa haki za binadamu miongoni mwa jamii na kwa baadhi ya viongozi wa vijiji, taasisi za umma na binafsi bado ni mdogo na kusema kuwa umma unahitaji kuhamasishwa kuhusu masuala ya haki za binadamu ili kupunguza vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu na Sheria mkoani humo.

Alisema kuwa vitendo vya uvunjwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora vimekuwa vinavyoripotiwa kila siku katika vyombo vya habari na vingine kutokea katika sehemu za kazi ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka, rushwa , unyanyasaji sehemu za kazi.

Makungu alisema vitendo hivyo vimepelekea baadhi ya viongozi na watumishi wakituhumiwa kwa kutumia vibaya madaraka yao, wizi wa mali za umma na ufisadi.

Aidha aliongeza kuwa ni vema elimu hiyo ikapelekwa maeneo ya vijijini ili kusaidia kuzuia uvunjifu wa haki za Watoto na wanawake ambao wamekuwa wahanga wa mateso na manyanyaso.

Makungua alisema baadhi ya wahanga wa vitendo viovu wamekuwa wakishindwa kupata haki zao kwani hawajui ni jinsi gani ya kutafuta haki hizo na kuwa na uelewa kuhusu vyombo vya utooaji haki na namna ya kuvifikia bado ni mdogo sana.

Alisema kuwa japokuwa Serikali imeanzisha madawati ya malalamiko katika sehemu za kazi lakini bado madawati hayo hayajafahamika kwa wananchi na kusema ipo haja ya kutoa elimu ya kuwawezesha kujua namna ya kudai haki na wapi ambapo mtu anaweza kudai haki hizo.

Nayea Afisa wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jovina Muchunguzi alisema mafunzo hayo yanalenga kutekeza mradi wa kuboresha upatikanaji haki kwa wote hususani wanawake katika mikoa yote nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages